Kimataifa

Italia yaongeza tahadhari dhidi ya maenezi ya Corona

March 11th, 2020 2 min read

Na AFP

ROME, ITALIA

ITALIA imeyatenga maeneo yote muhimu nchini humo, huku serikali ya taifa hilo ikichukua hatua za dharura kukabili maenezi ya virusi vya Corona.

Hili linamaanisha kuwa raia wake wote wamewekwa katika hali ya tahadhari.

Watu 463 wamefariki, huku wengine zaidi ya 9,000 wakiambukizwa virusi hivyo. Taifa hilo lina jumla ya watu 60 milioni.

Jana, Waziri Mkuu Giuseppe Conte alitangaza kwamba ataweka vikwazo kwenye shughuli za usafiri kote nchini. Vikwazo hivyo vilikuwa vimewekwa katika maeneo ya kaskazini pekee.

Hilo linajiri muda mfupi tu baada ya mamlaka za afya kutangaza vifo 97 vipya.

Italia pia ilitangaza kusimamisha shughuli zote za malipo ya nyumba, kulingana na Naibu Waziri wa Masuala ya Uchumi Laura Castelli.

“Naam, hivyo ndivyo tutakavyofanya kwa watu ambao wanalipa mikopo ya nyumba,” akasema waziri huyo, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Shirika la ABI, ambalo hutetea wadau mbalimbali katika masuala ya kiuchumi, lilisema kuwa hatua hiyo inafaa, kwani kuna haja ya kuzingatia afya za raia.

Italia ni nchi ya kwanza kuwaweka raia wake wote katika hali ya tahadhari kutokana na maenezi ya ugonjwa huo.

Kando na hayo, imesimamisha shughuli zote za michezo katika shule mbalimbali na vyuo vikuu. Vituo vya burudani pia vimefungwa.

Shughuli za kidini kama mazishi na harusi pia zimeahirishwa.

Nchini Ufilipino, Wizara ya afya ilitangaza visa vipya 11, hali iliyoongeza idadi ya watu walioathiriwa kuwa 35.

Rais Rodrigo Duterte ametangaza hali ya tahadhari, huku akitangaza kusimamisha shughuli zote za masomo kwa muda hadi Jumamosi.

Shughuli zingine za kijamii ambazo zimedhibitiwa ni ziara za kuwatembelea wagonjwa, wafungwa na tamasha zote za burudani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limeonya kwamba madhara ya virusi hivyo “yanazidi kulishtua.”

Nchini China, Rais Xi Jinping aliwasili kwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan, ambapo aliwatembelea maafisa wa afya wanaohusika kwenye shughuli za kukabili virusi hivyo.

Nchini Singapore, raia wa kigeni watalazimika kulipa, ikiwa watatibiwa dhidi ya maradhi hayo.

Wizara ya Afya nchini humo ilisema kuwa inatarajia ongezeko la maambukizi zaidi kuhusu visa hivyo.