Michezo

Ithibati tosha Diego Simeone anapenda wachezaji watundu

September 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Diego Costa amedhihirisha anapenda wachezaji watukutu baada ya kuongeza mshambuliaji Luis Suarez katika kikosi chake cha Atletico Madrid.

Suarez, 33, amejiunga na Atletico kutoka Barcelona mnamo Septemba 24 kwa Yuro milioni sita baada ya kuambiwa na kocha Mholanzi Ronald Koeman kuwa hamhitaji uwanjani Camp Nou.

Raia huyo wa Uruguay ni mshambuliaji hodari. Suarez ameondoka uwanjani Camp Nou baada ya kushinda Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2015 na Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mara nne, miongoni mwa mataji mengine.

Kwa kufunga mabao 198 tangu awasili Camp Nou mwaka 2013 akitokea Liverpool, Suarez anasalia mfungaji wa tatu bora wa Barca baada ya mshambuliaji wa Argentina Lionel Messi (634) na mwendazake Cesar Rodriguez (232).

Hata hivyo, Suarez anakumbukwa kwa vituko vingi uwanjani vikiwemo kuuma bega beki wa Italia Giorgio Chiellini katika Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil na pia kunyima Bara Afrika tiketi ya nusu-fainali alipopangua kichwa cha Dominic Adiyah kabla ya Asamoah Gyan kupoteza penalti Ghana ikiaga Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.

Simeone, ambaye enzi yake alikuwa beki shupavu katika klabu za Sevilla, Atletico Madrid, Inter Milan na Lazio, alisaini Diego Costa kutoka Chelsea mnamo Januari 2018.

Costa amegonga vichwa vya habari mara si haba kwa vituko. Akiwa Chelsea, mzawa huyo wa Brazil, ambaye ni raia wa Uhispania, aliwahi kusababisha mchezaji wa Arsenal Gabriel Paulista kuonyeshwa kadi nyekundu na pia alikanyaga vibaya Emre Can mguuni timu hiyo hiyo ikichuana na Liverpool. Pia, alipiga teke la kichwa beki wa Real Madrid Sergio Ramos katika kipute cha Uefa Super Cup.