Habari Mseto

Itumbi aachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu

July 10th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

MAHAKAMA imeamuachilia huru Dennis Itumbi kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu na kumuagiza awe akiripoti kila baada ya siku mbili kwa afisa anayechunguza tuhuma anazokabiliwa nazo na ambazo zinahusu kusambaza barua inayodaiwa kuwa ni feki iliyotoa madai ya kuwepo njama ya kumuua Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Mchunguzi ni afisa katika kituo cha polisi cha Muthaiga jijini Nairobi.

Itumbi vilevile ameagizwa asichapishe chochote kuhusu tuhuma zinazomkabili katika mitandao wa kijamii.

Dennis Itumbi ni nani?

Wale ambao wamewahi kukutana na kutangamana kwa muda mrefu na Dennis Itumbi katika maisha watakuambia kuwa ni mtu mgumu kumuelewa.

Mwandalizi wa makala haya amesoma naye kwa miaka mitatu katika Taasisi ya Mawasiliano ya Kufikia Watu Wengi, Kenya Institute of Mass Communication (KIMC) jijini Nairobi katika mtaa wa South B, akatagusana naye katika maisha ya kitaaluma kwa muda baadaye na cha mno, ni jirani katika Kaunti ya Kirinyaga.

Hayo tu ni ya kukufichulia kuhusu uwezekano wa makala haya kuchochewa na ama urafiki, ukaidi kwa mitazamo yake au tu umoja wa kimaoni kutokana na husiano hizo.

Kuna mhadhiri ambaye alimchambua Itumbi kama mwanamume aliye na ubongo wa kuandaa makubwa.

Naye mwingine alimtaja Itumbi kama “mwanasiasa mwanahabari ambaye hatawahi kutulia ndani ya vyombo vya habari bali ataishia kuwa mwanasiasa wa kawaida nchini.”

Atakayesema wahadhiri ni wajinga basi ajaribu kuchambua Itumbi katika msingi huo na utapata kuwa waligonga ndipo.

Lakini kisa kimoja ambacho kimebakia kuwa cha kurejelewa na wengi ambao walisoma naye KIMC ni wakati aliongoza wanafunzi wenza kuvamia mabweni ya wanafunzi kwa madai kuwa kuna maafisa wa serikali ambao walikuwa wamenyakua nafasi huko hivyo basi kusababisha msongamano wa malazi kwa wanafunzi.

Ubutu wa mawazo ya kitutu ni kuwa, sio wengi, hata ni kama hakukuwa aliyekuwa amefanya utafiti kujua waliokuwa wakiishi katika vyumba hivyo walikuwa kina nani.

Itumbi ni mjukuu wa Kasisi tajika nchini, Marehemu David Gitari.

Ilivyo ni kuwa, wanafunzi hao, mwandalizi wa makala haya akiwemo, wakiongozwa na Itumbi walijitokeza katika nyumba hizo na wakaanza kuwafurusha.

Lori la maafisa wa polisi kutoka kikosi cha kuzima ghasia liliingia kwa spidi ya juu katika lango kuu la mabweni hayo, maafisa wakiruka nje wakiwa wamejihami kwa mipini, bunduki na mabomu ya machozi.

Ni hapo ndipo mwandishi aliamua uoga sio laana; kujinusuru ni busara na hakuna kigezo cha kupima ujasiri ambacho kinazingatia kuwa kwanza uage dunia katika hali ambayo pengine baadhi watasema ni ya kijinga.

“Tusihepe! Umoja wa wanafunzi!” Itumbi alisikika akipiga nduru na mwandalizi huyu hakuwa mmoja wa wale waliotii wito wa Itumbi.

Asubuhi hii nyingine, katika habari za vyombo vya habari, nikiwa katika hifadhi ya nyumbani kwetu kijijini nilikosafiri moja kwa moja baada ya kufanikiwa kuhepa maafisa hao wa polisi, nilifahamu Itumbi alikuwa ametiwa mbaroni huku wanafunzi wenzake waliosimama naye wakiuguza majeraha kadhaa ya kutwangwa.

Kesi ya Itumbi mahakamani ilitamatika bila yake kufungwa jela; na baada ya miaka mitatu katika taasisi hiyo Itumbi akajiunga na vyombo vya habari huku na kule, akitoka kwa kasi baada ya kujiunga navyo na mara nyingi akionekana mitaani akisambaza Injili za kisiasa kwa waandishi wa habari wengine aliokuwa akiwafahamu.

Injili hizo zilikuwa ushawishi wa kuchapisha habari za kufaa mirengo aliyokuwa amejiunga nayo katika siasa, akiegemea kwa asilimia 100 kwa uwaniaji wa Mwai Kibaki katika uchaguzi mkuu wa 2007 na ule wa Rais Uhuru Kenyatta katika chaguzi za 2013 na 2017.

Leo hii, Itumbi yuko katika vyombo vya habari akihusishwa na kusambaza barua ambayo maafisa wanachunguza kama ni ‘feki’ na ambayo imesheheni ujumbe kwamba kuna njama ya kumuua Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Yeye hutajwa kuwa ni wa mrengo wa kuhakikisha Dkt Ruto anafika Ikulu katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Kwa hakika wanasiasa wamejitokeza wengi kumtetea akiwa kizuizini akichunguzwa kuhusu madai hayo.

Akiwa huru sasa kwa baada ya mahakama kumuachilia kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu aliyopewa na hakimu Zainab Abdul, ameponyoka ombi la upande wa mashtaka uliokuwa ukiomba kumzuilia kwa siku tisa zaidi katika kituo cha polisi cha Muthaiga.

Kwa sasa, atajitokeza mahakamani Julai 22 kutajwa kwa kesi yake.