Itumbi sasa aililia korti baada ya kudai kulikuwa na njama ya kumuua Ruto

Itumbi sasa aililia korti baada ya kudai kulikuwa na njama ya kumuua Ruto

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mkurugenzi wa mawasiliano ya dijitali katika Ikulu ya Nairobi Dennis Itumbi jana aliomba mahakama imwachilie huru katika kesi anayoshtakiwa kuchapisha habari za uwongo kuwa kulikuwa na njama za kumuua Naibu wa Rais Dkt William Samoei Ruto.

Bw Itumbi anayeshtakiwa pamoja na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa Bw Samuel Gateri kwa makosa ya kueneza habari feki katika mtandao wa Facebook aliilia korti imhurumie.

Na wakati huo huo Bw Gateri anayeshtakiwa pamoja na Bw Itumbi kwa kusambaza barua hiyo iliyodai kuna waziri aliyepanga njama za kumuua Dkt Ruto pia aliomba aachiliwe huru akidai hakuchapisha habari hizo zilizolenga kuzua vurugu.

“Polisi walikiri mbele ya mahakama kwamba hawakupata habari zozote katika mtandao wa Facebook wa Gateri kuhusu habari hizo za kumuua Dkt Ruto,” wakili Georgiadis Majimbo alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku.

Bw Majimbo alieleza korti Gateri alitiwa nguvuni kaunti ya Embu na polisi wa kupambana na uhalifu wa kimitandao hawakupata nakala ya barua iliyodaiwa aliisambaza katika mitandao ya kijamii akidai kulikuwa na njama za kumuua Dkt Ruto.

Wakili huyo alisimulia Gateri alikuwa ameorodheshwa kuwa shahidi ya Itumbi lakini polisi wakabadili nia walipodai barua hiyo iliyodaiwa ilikuwa na madai ya njama za kumwangamiza Ruto ilichapishwa katika mtandao wa Facebook wa mshtakiwa huyo kisha ikafutwa kabisa.

Kabla ya kufutwa kwa barua hiyo mahakama ilielezwa , ilielezwa tayari mitandao ya kijamii ilikuwa imeipata na kuisambaza kwa kasi kuu.

Barua hiyo ilidai mkutano ulifanywa katika hoteli ya Lamada na waziri katika serikali ya Jubilee ambapo yadaiwa walijadiliana jinsi ya kumtoa uhai Naibu wa Rais.

Mahakama ilielezwa na Bw Majimbo kwamba hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa kortini kuthibitisha madai hayo.

Korti iliombwa imwachilie Bw Gateri. “Ushahidi uliotolewa kortini ulithibitisha habari za uwongo za madai kulikuwa na njama za kumwangamiza Dkt Ruto zilienezwa katika mtandao wa vugu vugu la Tangatanga linalompigia debe naibu wa rais katika azma yake ya kutaka uongozi wa nchi hii baada ya kustaafu kwa Rais Uhuru Kenyatta Agosti 2022,” alisema Bw Majimbo.

Wakili huyo alisema mteja wake alikuwa ameorodheshwa kuwa shahidi dhidi ya Bw Itumbi.

Naye wakili Katwa Kigen anayemwakilisha Bw Itumbi alimsihi Bi Mutuku atupilie mbali kesi dhidi ya mwanablogi huyo akisema Kifungu nambari 66 cha Sheria za Kenya anachodaiwa alikaidi katika kusambaza katika mtandao wa Facebook barua hiyo ya madai ya kuuawa kwa Dkt Ruto kiliharamishwa na mahakama kuu.

Wakili Katwa Kigen anayemtetea Itumbi akiwa kortini…Picha/RICHARD MUNGUTI

“Mashtaka dhidi ya Bw Itumbi yamewasilishwa chini ya kifungu cha sheria kilichoharamishwa. Hivyo basi kesi dhidi ya Itumbi haiko chini ya sheria na naomba mahakama iifutilie mbali na kumwachilia chini ya kifungu cha sheria nambari 210 za uhalifu,” alisema Bw Kigen.

Kiongozi wa masjyaka Bw Anderson Gikunda aliomba mahakama ichambue ushahidi aliowasilisha kisha iwaweke washtakiwa hao wawili kizimbani wajitetee kwa vile walieneza uvumi wa uwongo kuhusu njama za kumuua Dkt Ruto katika mitandao ya kijamii.

Bi Mutuku atatoa uamuzi Septemba 15, 2021 iwapo washtakiwa watawekwa kizimbani kujitetea katika kesi ya kueneza habari za uwongo mnamo Juni 20 2019.

Washtakiwa walikanusha mashtaka na wako nje kwa dhamana.

  • Tags

You can share this post!

Mvutano mitandaoni baada ya Raila kutumia gari la serikali

Mbunge aalipa dhamana ya Sh100,000 kwa kumcharaza msanii