Michezo

Ivanovic avunja kombe la Russsian Cup akilinyanyua

July 27th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ALIYEKUWA mwanasoka matata wa Chelsea, Branislav Ivanovic alivunja bila kutarajia kombe la Russian Cup ambalo waajiri wake wa sasa Zenit St Petersburg walipokezwa baada ya kuwapepeta FC Khimki 1-0 kwenye fainali ya Julai 25, 2020 iliyopigiwa jijini Moscow.

Kombe liliponyoka mikononi mwa beki na nahodha huyo alipokuwa akilinyanyua juu kwa juu hewani. Lilidondoka chini baada ya takriban sekunde 30 pekee na kuvunjika vipande vipande.

Ililazimu wanasoka wa St Petersburg kusitisha sherehe yao kwa muda na kujaribu kuliunganisha upya kombe hilo lakini juhudi zao ziliambulia pakavu.

Jumbe za kumdhihaki Ivanovic na wenzake zilimiminwa na wapinzani pamoja na mashabiki wa washindani wao kwenye mtandao wa Twitter pindi baadaye.

Martin Ogilvie alisema: “Kuvunjika kombe ni jambo ambalo sijawahi kuliona katika historia ya soka. Sidhani ni jambo la busara. Wavihifadhi vipande vivyo hivyo kabatini mwao.”

“Sergio Ramos wa Real Madrid aliwahi pia kufanya hivyo akiwa juu ya basi lao wakati wa gwaride la heshima la kusherehekea ubingwa wao wa Klabu Bingwa Ulaya mnamo 2016-17,” akasema shabiki mwingine wa FC Khimki aitwaye George.

“Hakuwa na nguvu za kunyanyua taji hilo. Alionekana kuzidi na uzito tangu mwanzo. Huenda kombe hilo lilitengenezwa kwa nanga!” akaandika Jack Gregory.

Ivanovic, 35, aliingia katika sajili rasmi ya Zenit St Petersburg mnamo 2017. Alihudumu kambini mwa Chelsea kwa kipindi cha miaka tisa kati ya 2008 na 2017 na aliwahi kuwaongoza miamba hao wa soka ya Uingereza kunyanyua taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012. Beki huyo alisajiliwa na Chelsea kutokea Lokomotiv Moscow kwa kima cha Sh1.3 bilioni.

Video za kuonyesha kombe likiponyoka mikononi mwa Ivanovic kisha kuanguka sakafuni kutoka urefu wa futi saba na nusu na kuvunjika vipande vipande zimefutwa mitandaoni na kikosi cha Zenit St Petersburg kinachojiandaa kwa sasa kumsajili beki wa Liverpool, Dejan Lovren.