Makala

Ivory Coast ‘walivyobahatika’ kufika nusu fainali ya AFCON 2023, ndivyo watabeba Kombe?

February 4th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

WENYEJI wa Mashindano ya Kandanda ya Kombe la Taifa Bingwa Afrika (AFCON 2023) Ivory Coast wameendelea kupata ushindi wa ‘kimiujiza’ na sasa wameingia katika nusu fainali.  

Licha ya kusakata mechi dhidi ya Mali kwa muda mrefu wakiwa na wachezaji kumi, waliishia kuwabandua katika dakika ya mwisho.

Odilon Kossounou alilishwa kadi nyekundu mapema kwenye mechi baada ya kumchezea visivyo Lassine Sinayoko kabla ya Cote D’Ivoire kufungwa bao la mbali na Nene Dorgeles

Wenyeji, the Elephants, walisawazisha kupitia Simon Adingra na baadaye kufunga bao dakika ya 122 sekunde chache kabla ya refa kupuliza kipenga ili kumaliza mechi.

Ivory Coast wamekuwa wakicheza na kiwewe nywele zikisimama kichwani sababu hawajakuwa na makali kinyang’anyironi.

Walipoteza mechi mbili za makundi na kuaga mashindano wakisubiri pengine wataingia raondi ya 16 kama timu bora namba tatu.

Walibahatika kuchukua nafasi nne za ziada baada ya Morocco ‘kuwasaidia’ kwa kupiga Zambia waliokuwa na nafasi nzuri zaidi ya Ivory Coast.

Kocha wao Jean-Louise Gasset alipigwa kalamu na kaimu mkufunzi Emerse Fae amekuwa akishinda kiajabuajabu.

Dhidi ya bingwa mtetezi Senegal, Ivory Coast ililazimisha sare dakika ya mwisho na baadaye kuwatwanga katika mikwaju ya matuta walipomenyana mkondo wa mtoano.

Ifikapo Februari 7, Ivory Coast watapimana nguvu na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) katika nusu fainali.

Nao Nigeria watagaragazana na Afrika Kusini, waliowabandua Cape Verde, kujua nani ataingia fainali ya AFCON 2023