Habari Mseto

Jachinga azikwa usiku wa manane

June 13th, 2020 1 min read

NA RUSHDIE OUDIA

Mwanamuziki Bernard Onyango anayejulikana kama Abenny Jachinga alizikwa usiku wa manane.

Jachinga, aliyefariki Alhamisi alizikwa na polisi Jumamosi saa nane za usiku, huku nduguye mdogo akiruhusiwa kumwona pekee.

Vita vilizuka kati ya polisi na wenyeji Ijumaa mamia ya waombolezaji huku wakirushia polisi mawe. Waombolezaji hao walikuwa wanataka kuuona mwili wa mwendazake na kumpa heshima za mwiso kabla ya kuzikwa.

Walitoa jeneza kutoka kwa kaburi ambapo polisi walikuwa tayari wameshaliteremsha kumzika msanii huyo.

Baada ya kulitoa geneza hilo, walizunguka nalo kijijini baada ya kupeleka mwili kwenye chumba cha kuhifadhi maiti kilicho karibu.

Saa saba na dakika arubaini hivi Jumamosi usiku polisi waliutoa mwili wa marehemu kutoka mochari na wakapeleka mwili huo na kuuzika nyumbani mwa mwimbaji huyo.