Michezo

JACK OCHIENG: Kocha nguli nchini na Afrika Mashariki

August 24th, 2020 2 min read

JOHN KIMWERE, NAIROBI

TANGU aanze kunoa timu ya Nairobi Water ameibuka miongoni mwa makocha wanaolenga makuu katika mchezo wa handiboli barani Afrika.

Ufundishaji wake wa kipekee imeimarisha mchezo wa klabu hiyo ya kina dada pakubwa hadi kuzima wapinzani wao hapa nchini bila kuweka katika kaburi la sahau katika ukunda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwa jumla.

Nairobi Queens imeibuka moto wa kuotea mbali kwenye kampeni za Ligi Kuu nchini iliyotawaliwa na kikosi kilichokuwa mashuhuri cha Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Hakika kocha Jack Herbert Ochieng hakika anapania kufikia hadhi kubwa katika handiboli ya wanawake barani.

Kocha huyo anasema licha ya pandashuka za kiufadhili wanazopitia analenga kubeba ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika (CAHB). Anasema wamepania kuimarisha mchezo wao kwenye ngarambe hiyo maana mwisho waliposhiriki mwaka 2016 walimaliza nafasi ya tano.

JUMUIYA YA MADOLA

“Binafsi nilianza kushiriki handiboli nilipotinga miaka 16 ambapo miaka miwili baadaye niliteuliwa kujiunga na timu ya taifa niliyoichezea kwa muda mrefu,” Ochieng aeleza. Anaongeza, “Nimezuru mataifa kama Uingereza kati ya mengine mengi nikichezea timu ya taifa kwenye mashindano tofauti kama Jumuiya ya Madola kati ya mengine.”

Akiwa mchezaji aliwakilisha Kenya mara tano kwenye dimba la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati. Alianza kunoa timu ya madume ya Black Mamba mnamo 2000, baada ya kuichezea kwa miaka 15.

MARA SABA

Umahiri wake umechangia timu hiyo kuibuka mpinzani mkuu kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (ECAHF) huku ikijivunia kuhifadhi taji hilo mara saba muhula uliyopita kwenye michezo iliyoandaliwa Amahoro Stadium mjini Kigali, Rwanda.

Ilihifadhi taji hilo ilipokomoa Winners ya Rwanda mabao 43-13 kisha kubamiza Rwanda Univesity kwa mabao 38-26. Kwenye utangulizi wa mechi hizo, Nairobi Water ilikomoa Winners mabao 43-13 kisha ilibamiza Rwanda Univesity kwa mabao 38-26.

Kwenye patashika ya malkia hao na Rwanda University, wafungaji bora walikuwa Brenda Ariviza aliyefunga mabao 12 nao Melvin Akinyi na Brenda Musambai kila mmoja alitikisa wavu mara sita. “Kwa jumla timu za Afrika Mashariki hazina uwezo tosha kudhibiti zitokazo mataifa ya Magharibi mwa Afrika,” asema.

Katika mpango mzima usongora wake umechangia kuteuliwa kocha wa timu ya taifa.

SUPER CUP

Anaongeza kuwa klabu za wanaume na wanawake humu nchini zinahitaji mbinu mpya ikiwemo kushiriki mechi za kirafiki dhidi ya wenzao kutoka Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo, Morocco na Cameroon kati ya mataifa mengine.

Ochieng ameongoza Nairobi Water kushinda taji la Super Cup mara tano kwenye mashindano ambayo huandaliwa kabla ya mechi za Ligi Kuu kukunjua jamvi.

Ameongoza kina dada kubeba taji la Ligi Kuu mara sita. Anasisitiza kuwa kukuza timu imara unahitaji kuanza na wachezaji chipukizi.