Makala

Jackie Matubia: Wanawake Wakenya wanapenda wanaume wakorofi

April 9th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO

‘TOXIC’, ambayo ni filamu iliyoandaliwa na kusukwa na mwigizaji staa Jackie Matubia, itaingia sokoni Aprili 17, 2024.

Ni telenovela itakayoangazia misukosuko ya kimapenzi hasa kwa mademu (wapenzi) wa mjini.

Matubia na mwigizaji Mike Saruni ndio watakaokuwa wahusika wakuu.
Chaguo la kumpa uhusika mkuu Saruni linatokana na sababu kwamba watayarishaji wa Toxic walihisi kuwa ndiye atakayeweza kuvalia kisawasawa uhusika wa mwanamue mwenye mvuto na sura ya kikorofi.

“Mike anavalia uhusika wa jamaa mmoja mwenye sura na mvuto anayejua kubeza mademu kwelikweli, ila kiuhalisia anaishi kuwachezea na mwisho wa siku anawavunja moyo. Ni mwanamume mkorofi siyejali hisia za mwanamke, ni mwanamume mtesi wa hisia,” anaeleza Matubia.
Matubia anasema chaguo la Saruni lilifikiwa naye pamoja na mwandishi wa telenovela hiyo, marehemu mwigizaji na produsa Charles Ouda.
Charles Ouda alifariki dunia Februari mwaka huu (2024) kwa kile kilichoripotiwa kuwa ni kujitia kitanzi.
“Wakati Charlie alikuwa anaiandika shoo hii, akilini alikuwa anawaza mwanamume sukari ya warembo ila mkorofi sana. Hachelewi kuwaumiza na hata akiwaumiza, bado wanaamua kubakia naye. Wazo lilitokana na  uwepo wa mtazamo kuwa wanawake wengi wa Kikenya wanapenda wanaume wa aina hii, wanaume ambao ni stresi tupu, na kwenye misingi hiyo tuliyemwona anatosha kuibeba picha hiyo kikamilifu ni Saruni,” Matubia kaongezea.
charles Ouda na Jackie Matubia walikuwa ni maswahiba wa kufa kuzikana na mara nyingi walionekana pamoja.

“Toxic ndio mradi tuliokuwa tukiuhangaikia kabla Ouda afariki dunia. Alipofariki nilichanganyikiwa kidogo maana sikujua kama niendelee na mradi wenyewe au itakuwaje maana yule tuliyekuwa tukisaidia naye hayupo tena. Ila niliwaza na kuamua kuendelea maana naamini ndio uamuzi ambao angelipenda niufanye.”

Jackie Matubia, kando na kuwa mwigizaji, ni mshawishi wa kimitandao.

Msanii huyu ameshinda tuzo kadha katika tasnia ya uigizaji filamu.