Habari Mseto

Jackpot ya Sh208 milioni kwa mwanasiasa aliyewania ubunge na kubwagwa

October 1st, 2018 1 min read

NA MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA mwaniaji wa ubunge wa Konoin, Kaunti ya Bomet amejiunga na kundi la mamilionea baada ya kushinda Sh208 milioni katika shindano la Sportpesa.

Bw Cosmas Korir, mkurugenzi wa sasa wa Kilimo katika Kaunti ya Pokot Magharibi alishinda Sh208,733,619 milioni, mnamo Jumapili.

“Ni kweli nimeshinda Jackpot ya Sportpesa. Nasubiri kuambiwa na Sportpesa kuhusu jinsi ya kuchukua fedha hizo,” Bw Korir aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Alipoulizwa atakachofanyia fedha hizo, Bw Korir alisema “Sijaanza kufikiria namna ya kutumia fedha hizo. Bado sijaamini kwamba nimeshinda kiasi hicho cha fedha.”

Aliongeza, “Namshukuru Mungu kwa kunipatia kiasi hicho cha fedha; nina furaha isiyo na kifani.”

Bw Korir alisomea Kilimo katika Chuo Kikuu cha Egerton.

Amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Kilimo katika Kaunti ya Bomet chini serikali ya gavana wa zamani Isaac Ruto.

Bw Korir aliwania ubunge kwa kutumia Chama cha Mashinani (CCM) lakini akabwagwa na Bw Brighton Yegon wa Jubilee.