Habari

Jacque Maribe atumwa Mathari kupimwa akili

October 9th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MTANGAZAJI wa runinga Jacque Wanjiru Maribe Jumanne alitumwa kupimwa akili kabla ya kushtakiwa rasmi kwa mauaji.

Bi Maribe aliamriwa apelekwe hospitali ya kutibu wendawazimu ya Mathari kuchunguzwa utimamu wa akili yake kabla ya kujibu shtaka la kumuua Monicah Kimani.

Mtangazaji huyo alifikishwa mbele ya Jaji Jessie Lesiit akiwa na mchumba wake Joseph Irungu alimaarufu Jowie.

Jowie alikuwa na bandeji katika moja ya mabega yake kutokana na jeraha la risasi. Wote walisimama kizimbani na kufahamishwa shtaka dhidi yao.

Jaji Lesiit aliwafahamisha wapenzi hao wanakabiliwa na shtaka la kumuua Monicah Kimani katika mtaa wa Kilimani, Kaunti ya Nairobi.

“Hamhitaji kujibu shtaka dhidi yenu.Nitawajulisha tu. Nawafahamisha tu muelewe sababu mmfIkishwa kortini,” Jaji Lesiit aliwaeleza wapenzi hao.

Baada ya kuwaeleza shtaka dhidi yao, Jaji Lesiit alimwuliza kiongozi wa mashtaka Bi Catherine Mwaniki ikiwa amewasilisha kortini ripoti kuhusu hali ya akili ya washukiwa hao wawili.

“Niko na ripoti ya Irungu. Mtaalamu wa tiba za akili amesema yuko na akili timamu. Anaweza kusomewa shtaka,” alisema Bi Mwaniki.

Bi Mwaniki aliongeza, “Sina ripoti ya mshukiwa wa pili (Maribe). Naomba nipewe muda apelekwe hospitali ya Mathari kupimwa.”

Ombi hilo la Bi Mwaniki lilipata upinzani mkali huku wakili Katwa Kigen anayemwakilisha Bi Meribe akisema, “hata hii mahakama inaona mshukiwa huyu yuko na akili timamu. Yuko sawa kabisa.”

Bw Kigen alisema mpeperushaji matangazo huyu amekuwa rumande kwa siku 10 na polisi.

“Polisi wamemzuia mteja wangu kwa siku 10. Kitu gani kiliwazuia kumpeleka hospitali kupimwa?” alihoji wakili Kigen.

Bw Kigen anayemtetea Bi Maribe akiwa na Bw Dunstan Omar aliomba mshukiwa huyo apelekwe kupimwa akili leo (jana) alasiri kisha arudishwe mahakamani baadaye kujibu shtaka.

“Hakuna namna mmoja wa washukiwa hawa wanaoshtakiwa pamoja anaweza kusomewa shtaka akiwa peke yake. Sheria inaamuru wanaoshtakiwa pamoja wasomewe pamoja,” alisema Jaji Lesiit.

Mawakili Cliff Ombeta , Samson Nyaberi na Magati Laichema wanaomwakilisha Jowi waliomba mahakama imsomee shtaka kwanza kisha na Bi Maribe baadaye ripoti ya mtaalamu wa tiba ya akili ikiwasilishwa.

Mshukiwa Joseph Irungu asema na wakili wake Cliff Ombeta mahakamani Oktoba 9, 2018. Picha/ Richard Munguti

Jaji Lesiit aliamuru mshukiwa huyo apelekwe Mathari kupimwa akili na ripoti iwasilishwe kortini Oktoba 15 2018.

Jaji aliamuru washukiwa hao wazuiliwe na idara ya magereza.

“Kabla ripoti hiyo kuwasilishwa itabidi mkae ndani,” alidokeza Jaji Lesiit.

Alimwamuru Jowi azuiliwe katika gereza la Viwandani naye Bi Maribe apelekwe katika gereza la wanawake la Langata.

Mawakili wa Bw Irungu waliomba aachiliwe kwa dhamana wakisema, “anahitaji matibabu maalum kutokana na jeraha la risasi begani.”

“Tuko na ripoti kutoka hospitali ya Nairobi West kwamba mshtakiwa apelekwe hospitali kuu ya Kenyatta (KNH) kupata matibabu maalum,” alirai Bw Nyaberi.

Mahakama iliamuru mshukiwa azuiliwe na iwapo kutazuka haja ya kupata matibabu maalum idara ya magereza itamshungulikia.

Jaji Lesiit alimwamuru Bw Nyaberi amkabidhi DPP nakala za ombi hilo la dhamana ndipo afisa anayechunguza kesi ajibu tetezi za mshtakiwa.

Washtakiwa watafikishwa mahakamani tena Oktoba 15 kusomewa shtaka.

Wawili hawa walitiwa nguvuni na uchunguzi ukaanza kufanywa mara moja kubaini jukumu walilotekeleza katika mauaji ya Bi Kimani.

Bi Kimani alikuwa mfanyabiashara nchini Sudan Kusini.