Habari

Jacque Maribe kufanyiwa uchunguzi wa DNA kuhusu mauaji

October 1st, 2018 2 min read

BENSON MATHEKA Na ERIC WAINAINA

MWANAHABARI Jacque Wanjiru Maribe, anayechunguzwa kuhusiana na mauaji ya Monica Nyawira Kimani, atafanyiwa uchunguzi wa vinasaba vya damu (DNA) ili kulinganisha matokeo watakayopata polisi kutokana na sampuli walizokusanya kutoka nyumba yake iliyoko Royal Park, Lang’ata jijini Nairobi na katika nyumba ya marehemu eneo la Milimani.

Jumatatu, Bi Maribe na jirani yake Brian Kasaine walifikishwa katika mahakama ya Kiambu ambapo polisi waliruhusiwa kuwazuilia kwa siku 10 zaidi ili waweze kukamilisha uchunguzi.

Inspekta wa polisi Maxwel Otieno anayeongoza uchunguzi huo, alisema kupitia hati ya kiapo kwamba simu ya Bi Maribe ilitwaliwa na polisi ili kufanyiwa ukaguzi ambao unaendelea. “Simu ya mshukiwa aina ya iphone 7 ilitwaliwa ili kukaguliwa na ripoti haijakuwa tayari, na inaaminika kuwa ina ushahidi kuhusiana na kesi inayochunguzwa,” Bw Otieno aliambia Hakimu Mwandamizi wa Kiambu Justus Kituku.

Bw Otieno pia alisema akiwa mtangazaji maarufu wa runinga, Bi Maribe anaweza kuingilia uchunguzi.

Alisema polisi wanaamini kwamba mwanahabari huyo alikuwa pamoja na mshukiwa mkuu Joseph Irungu Kuria, ambaye pia ni mpenzi wake.

Kuhusu Kasaine, mahakama iliambiwa kwamba alimpatia Bw Irungu bastola ambayo inashukiwa alitumia kujipiga risasi ndani ya nyumba ya Bi Maribe. “Uchunguzi umefichua kwamba mmoja wa washukiwa mara kwa mara alimpatia Bw Joseph Irungu silaha yake na moja ya siku hizo ni Septemba 8, 2018,” Bw Otieno anaeleza kwenye hati yake iliyowasilishwa mahakamani jana.

Polisi walitwaa viatu na nguo kutoka nyumba ya Bi Maribe ambavyo wanataka kufanyia uchunguzi kabla ya kuamua iwapo watamfungulia mashtaka.

“Kufikia sasa uchunguzi wa mwanzo umeonyesha kwamba Bw Irungu alionekana na mtu mwingine eneo ambalo uhalifu ulitendwa akiendesha gari la Bi Maribe.

Mahakama ilikubaliana na upande wa mashtaka ikisema kulikuwa na sababu za kuridhisha kuendelea kumzuilia Bi Maribe lakini ikawapa polisi siku 10 badala ya 14 walizokuwa wameomba.

Iliagiza azuiliwe katika kituo cha polisi cha Gigiri naye Kasaine azuiliwe katika kituo cha polisi cha Lang’ata. Irungu anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.