Michezo

Jadon Sancho atozwa faini kwa kunyolewa bila barakoa

June 7th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHIPUKIZI Jadon Sancho wa klabu ya Borussia Dortmund amepigwa faini na vinara wa soka ya Ujerumani baada ya kuonekana akinyolewa bila ya kuvalia barakoa.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye ni mzawa wa Uingereza alionekana kwenye picha na mchezaji mwenzake, Manuel Akanji ambaye pia amepigwa faini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wasimamizi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (DFL), “wawili hao walikuwa wamekiuka kanuni za kimsingi za afya na kujikinga kwao hakukufikia viwango inavyotakikana.”

Hata hivyo, Dortmund iliwatetea wanasoka hao vikali kwa kusisitiza kwamba hawakuwa wamevunja masharti yoyote kati ya sheria za afya zinazodhibiti soka ya Bundesliga.

Gazeti la Bild nchini Ujerumani lilipakia kwenye mtandao wa Twitter habari na picha zilizowaonyesha Sancho na Akanji wakiwa karibu sana wakati wa kunyolewa.

Mnamo Juni 5, 2020, Michael Zorc ambaye ni Mkurugenzi wa Spoti kambini mwa Dortmund alisema Sancho na Akanji walikuwa miongoni mwa wanasoka sita kambini mwao waliohakikishia uongozi kwamba walikuwa wamezifuatilia kanuni zote za afya na barakoa walizokuwa wamevalia zilitolewa tu wakati wa kupigwa picha.

Ingawa hivyo, DFL iliamua kuwaadhibu Sancho na Akanji kwa kutokuwa na chochote cha kutojikinga dhidi ya virusi vya homa kali ya corona.

“Tunatambua kwamba wanasoka wana ulazima wa kunyolewa. Lakini hili ni jambo ambalo linastahili kufanywa chini ya kanuni zote za afya katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19,” ikasema sehemu ya taarifa ya DFL.