Michezo

Jagina Mkorea afa katika mbio za kilomita 10 Nyahururu

January 14th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKIMBIAJI Yoo Byungwon aliaga dunia katika mbio za barabarani za kilomita 10 za Nyahururu nchini Kenya mnamo Januari 13, 2019.

Inasemekana raia huyo wa Korea Kusini mwenye umri wa miaka 61, ambaye aliwasili nchini Januari 8 kushiriki makala haya ya pili, alikuwa akijaribu kutimka umbali wa kilomita 42.

Alifariki mara tu alipowasili katika hospitali ya kibinafsi. Alikuwa amesimama kwa ghafla katika mashindano haya na kuanza kutetemka akiishiwa na pumzi kabla ya kuanguka chini.

Inasemekana kabla ya kuanguka chini katika eneo la mashindano la Maili Saba, Byungwon alionekana mwenye furaha na hata kupungia mkono mashabiki waliokuwa kando ya barabara.

Kisa hiki kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Nyahuruhu, huku Ubalozi wa Korea jijini Nairobi pamoja na jamaa zake wakifahamishwa yaliyomfika.

Mwili wake ulisafirishwa hadi jijini Nairobi kuhifadhiwa huku jamaa zake wakisubiriwa kuamua kama atachomwa jijini Nairobi ama nchini Korea.