Jagina wa soka kambini mwa Bayern na Ujerumani, Gerd Muller afariki akiwa na umri wa miaka 75

Jagina wa soka kambini mwa Bayern na Ujerumani, Gerd Muller afariki akiwa na umri wa miaka 75

Na MASHIRIKA

ALIYEKUWA jagina wa soka kambini mwa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Gerd Muller ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Fowadi huyo alifunga mabao 68 kutokana na mechi 62 akivalia jezi za Ujerumani, likiwemo goli lililoshindia taifa hilo ufalme wa Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi mnamo 1974.

Muller aliwahi pia kuhudumu kambini mwa Bayern kwa miaka 15 na akaweka rekodi ya kufunga mabao 365 kutokana na mechi 427 za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

“Leo ni siku ya huzuni kwa FC Bayern Munich na mashabiki wao wote. Muller ndiye mshambuliaji wa haiba kubwa zaidi kuwahi kuhudumu kambini mwa Bayern. Tunaombea familia yake wakati huu,” akasema rais wa Bayern, Herbert Hainer.

Muller aliwahi kutawazwa Mfungaji Bora wa Kombe la Dunia mnamo 1970 baada ya kufunga mabao 10 katika fainali hizo na akatwaa taji la Ballon d’Or mwaka huo. Aliongoza Ujerumani kunyanyua taji la Euro miaka miwili baadaye.

Alishikilia rekodi ya kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kupachika wavuni magoli 85 mnamo 1972 hadi Messi alipompita mnamo 2012.

Rekodi yake ya mabao 40 katika msimu mmoja kwenye kampeni za Bundesliga ilidumu kwa miaka 49 kabla ya kuvunjwa na mshambuliaji wa Bayern, Robert Lewandowski mnamo Mei 2021.

Kwa ujumla, Muller alifungia Bayern mabao 566 kutokana na mechi 607 na akasaidia kikosi hicho kushinda mataji manne ya Bundesliga na DFB, makombe matatu ya European Cup, European Cup Winnres’ Cup na Intercontinental Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Watu 20 waangamia katika mlipuko wa tangi la mafuta Lebanon

TAHARIRI: Mauaji ya vijana yatia hofu