Habari

Jaguar kuzuiliwa kwa siku tatu zaidi

June 28th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI na MAUREEN KAKAH

MBUNGE wa Starehe Charles Njagua atazuiliwa kwa siku tatu zaidi katika kituo cha polisi cha Kileleshwa baada ya mahakama kusema kuna haja ya kulinda uchunguzi unaoendeshwa kuhusu matamshi aliyotoa yanayosawiriwa kama uchochezi.

Ingawa Hakimu mkazi wa mahakama jijini Nairobi, Tobiko Sinkiyan amesema haijathibitishwa ni vipi Njagua atavuruga uchunguzi, amesema bila shaka mbunge huyo ambaye pia wengi wanamjua kama Jaguar ni mtu mwenye ushawishi.

Hivyo hakimu alisema hakuna tashwishi kwamba ipo haja ya kulinda na kuhifadhi ripoti ya uchunguzi.

Alhamisi maafisa wa polisi walikuwa wameomba azuiliwe kwa siku 14 katika kituo cha polisi cha Kamukunji.

Jaguar alikamatwa Jumatano ikiwa ni siku chache baada ya kutoa matamshi akitaka wafanyabiashara wa kutoka mataifa ya kigeni hasa wa Tanzania na China wafurushwe.