Habari Mseto

Jaji akosoa jamii kwa kusamehe wabakaji badala ya kuwashtaki

January 31st, 2019 1 min read

Na Pius Maundu

JAJI wa Makahama Kuu ya Makueni, Bw Charles Kariuki amesema mtindo wa kuwatumia wazee kusuluhisha kesi za ubakaji umekuwa kikwazo kwa vita vinavyolenga kutokomeza dhuluma hiyo katika jamii.

Bw Kariuki alisema visa vya ubakaji vinazidi kuongezeka na kuwataka wenyeji kufikisha kesi hizo mahakamani, ili wahusika waadhibiwe kisheria badala ya kushirikiana na wazee pamoja na jamaa za familia kuwapa msamaha.

“Njia mbadala haifai kutumika kusuluhisha visa vya ubakaji au dhuluma za kimapenzi ,” akasema Jaji huyo katika soko la Nunguni wakati wa siku ya kutangamana na kuweka wazi shughuli za mahakama ya Kilungu kwa umma.

Walioongea katika hafla hiyo walilalalama kuwa ni visa vichache vya ubakaji vinavyoripotiwa, na vingi hulekwa kwa wazee.

Kulingana na Hakimu mkaazi mkuu wa mahakama ya Kilungu Charles Mayamba, taasisi hiyo imepata sifa kwa kushughulikia kesi za unajisi haraka. Alifichua kwamba wabakaji 48 walipokezwa vifungo vya kati ya miaka 15 na wengine kutumikia vifungo vya maisha mwaka uliopita.

Hili lilikuwa ongezeko kubwa kutoka kwa wabakaji 22 waliofungwa mwaka wa 2017, ishara tosha kwamba gurudumu la haki haliwasazi wanaoshiriki tabia hiyo mbovu.

Afisa Mkuu wa Kaunti ya Makueni anayesimamia jinsia Diana Muli naye alisifu mwenendo mpya wa jamii kuchangamkia mahakama katika kutatua kesi za unajisi kwa kuziwasilisha katika mahakama ya Kilungu.

“Ili kushinda vita dhidi ya ubakajji, tunafaa kuendelea kuwafichua na kuwaripoti wanaohusika,” akasema wakati wa hafla hiyo.