Jaji aliyemzima Mwilu amrudisha kuwa Kaimu Jaji Mkuu

Jaji aliyemzima Mwilu amrudisha kuwa Kaimu Jaji Mkuu

Na RICHARD MUNGUTI

KAIMU Jaji Mkuu Philomena Mbete Mwilu amerudishwa kazini baada ya Mahakama Kuu ya Meru kusitisha maagizo iliyotoa Ijumaa.

Maagizo hayo ya Ijumaa yalisambaratisha shughuli zote za idara ya mahakama. Katika maagizo hayo ya Ijumaa, Jaji Patrick Jeremy Otieno alikuwa amemzima kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kutekeleza majukumu matano ya Idara ya Mahakama.

Lakini Jumatatu, Jaji Otieno alifutilia mbali agizo alililotoa na kuamuru tena Jaji Mwilu arejelee majukumu yake ya kuendelea kuwa kaimu Jaji Mkuu, Naibu wa Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Juu na kuongoza vikao vya Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC).

Pia Jaji Mwilu ataendelea kupokea malalamishi dhidi ya watumishi wa idara ya mahakama. Jaji huyo aliamuru agizo kesi dhidi ya Jaji Mwilu isikizwe Februari 12, 2021.

“Maagizo ya Ijumaa ya kumzuia Jaji Mwilu akitekeleza majukumu yake yameondolewa. Kesi iliyowasilishwa na chama cha wanasheria nchini LSK pamoja na ile iliyowasilishwa na mkazi wa Maua, Meru Mwongela Isaiah Mbiti itasikizwa Februari 12, 2021,” aliamuru Jaji Otieno.

Jaji huyo aliamuru wahusika wawasilishe ushahidi. Uamuzi huo wa Ijumaa ulitumbukiza Idara ya Mahakama katika hali ya kuchanganyikiwa.

Kutupwa kwa agizo hilo la Ijumaa sasa kumerejesha hali ya utulivu kortini kwa vile sasa Mahakama ya Juu inaweza kusikiza kesi kwa vile Jaji Mwilu pamoja na Majaji Mohammed Ibrahim, Njoki Ndung’u , Smokin Wanjala na Isaac Lenaola wanaweza kuendesha vikao.

Miongoni mwa kesi zilizokuwa zimeathirika ni ile ya uteuzi wa Anne Kananu Mwenda kuwa Naibu wa Gavana wa Nairobi.

Kesi nyingine ambayo iliathiriwa ni ile Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana kuomba ufafanuzi ikiwa katiba inaweza kurekebishwa kupitia mchakato wa BBI.

Katika kesi iliyowasilishwa mahakama kuu ya Meru na wakili Aulo Soweto na Jack Awele, Jaji Mwilu alieleza waziwazi kwamba malalamishi ya Bw Mwongela yalishughulikiwa na majaji watano wa mahakama kuu waliotupilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Geoffrey Kinoti kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

Mbali na kesi hizo zilizo mbele ya JSC, mwanaharakati Okiya Omtatah pia amewasilisha kesi akiomba Jaji Mwilu azuiliwe kuwa kaimu Jaji Mkuu.

Jaji Mwilu atapambana kufa kupona kujinasua katika kesi dhidi yake na kuwania wadhifa wa Jaji Mkuu alioutangaza wazi Januari 12,2021 baada ya kustaafu kwa Bw David Maraga baada ya kuhitimu miaka 70.

Endapo Jaji Mwilu atateuliwa kuwa Jaji Mkuu atahudumu kwa kipindi cha miaka minane kwa vile sasa yuko na umri wa miaka 62.

Jaji Mwilu alikabidhiwa hatamu za kuwa kaimu Jaji Mkuu na David Maraga aliyestaafu Januari 11, 2021.

You can share this post!

Rais awaongoza vigogo wa siasa kumwomboleza Nyachae

Homeboyz wakiri ni pigo kwao kupoteza wanaraga wanne