Jaji aliyetimuliwa adai alitemwa bila utaratibu

Jaji aliyetimuliwa adai alitemwa bila utaratibu

Na SAM KIPLAGAT

JAJI wa Mahakama Kuu, Martin Muya amesema, Tume ya Huduma kwa Mahakama (JSC) ilimsimamisha kazi bila kufuata utaratibu ufaao.

Bw Muya jana aliambia majaji watano wa Mahakama ya Juu kwamba, JSC ilimsimamisha kazi bila mlalamishi kuwasilisha rasmi barua mbele ya tume kulingana na matakwa ya sheria.Wakili wake Philip Nyachoti alisema kuwa, mlalamishi alifika mbele ya Jaji Mkuu David Maraga (ambaye sasa amestaafu).

“Jaji Mkuu baadaye aliandikia barua JSC akitaka ichunguze madai hayo.“Barua hiyo ya Maraga haikuwa malalamishi rasmi kwa JSC kwani Katiba imeelezea wazi utaratibu wa kumtimua jaji,” akasema.

Bw Nyachoti pia alisema Jaji Muya hakupewa fursa ya kujitetea kwa kuwa faili ya malalamishi dhidi yake haikupelekwa mbele ya JSC na jopo lililobuniwa kumchunguza.

“Faili hiyo ilikuwa muhimu kwani ingemwezesha kujiandaa na kujibu madai yote yaliyotolewa dhidi yake. Aliendelea na kesi hiyo kwa sababu alilazimishwa,” akasema.

Jopo maalumu lililoongozwa na Jaji Alnashir Visram ilimpata Jaji Muya na hatia ya utovu wa maadili kutokana na hatua yake ya kuchelewesha kusoma hukumu kwa miezi mitano.Kesi iliyomuweka pabaya ilihusisha benki ya NCBA na duka la Kipsigis Stores.

Benki ya NCBA ilitaka kupiga mnada malori 14 ya Kipsigis Stores ambayo duka hilo lilitumia kama dhamana kuchukua mkopo.

Lakini Benki ya NCBA ilipoenda kupiga mnada malori hayo, ilipata tayari yamepigwa mnada na benki nyingine kuhusu mkopo.

Jaji Muya alizuia Benki ya NCBA kutochukulia hatua duka la Kipsigis Stores bila kutoa sababu. Agizo hilo lilisababisha benki hiyo kupoteza Sh76 milioni.

Bw Nyachoti jana aliambia Majaji wa Mahakama ya Juu; Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u Isaac Lenaola na Willian Ouko kwamba mlalamishi alikataa kukata rufaa hata baada ya kuwapa fursa hiyo.

“Mlalamishi alichagua kutokata rufaa ilhali jaji alimtaka kufanya hivyo iwapo hakuridhishwa na uamuzi,” akasema.Jaji huyo pia alidai kuwa alichelewesha hukumu kwa sababu alikuwa akihudumu katika vituo viwili mjini Bomet na Kericho.

Wakili Munene Eredi aliyewakilisha Mwanasheria Mkuu, alisema kuwa Jaji Muya hakuwasilisha ushahidi wa kuonyesha kwamba alikuwa akifanya kazi Bomet na Kericho.

You can share this post!

Pigo kwa afisa korti kuunga uamuzi wa gavana kumfuta

Jumwa aonywa UDA itazima nyota yake