Habari Mseto

Jaji apinga Rais akiteua jopo la kumchunguza

May 27th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MMOJA wa majaji watatu ambao majina yao yalipelekwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ateue majopo ya kuwachunguza kwa utovu wa nidhamu na ufisadi ameishtaki Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC).

Jaji Martin Muya, anayehudumu katika mahakama kuu ya Bomet aliishtaki JSC akisema hakuridhishwa na uamuzi huo.

Jaji Muya anaomba mahakama kuu ibatilishe uamuzi huo na kuzuia uteuzi wa jopo kumchunguza hadi suala hilo liangaziwe upya na JSC.

Jaji huyo aliwasilisha kesi katika mahakama kuu akiomba lisikizwe kwa dharura kabla ya jopo kuteuliwa na hatimaye kutimuliwa kazini.

Jaji Muya pamoja na Majaji Lucy Waithaka na D K Marete walipatikana na hatia ya utovu wa nidhamu na ufisadi na JSC kisha majina yao yakapelekwa kwa Rais Kenyatta kuteua majopo ya kuwahoji na kutoa uamuzi iwapo waachishwe kazi ama warudishwe kazini.

Mnamo mwaka wa 2003, Jaji Muya alikuwa miongoni mwa mahakimu 83 waliotimuliwa kazini baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu Evan Gicheru kupokea ripoti ya jopo iliyochunguza uozo katika idara ya mahakama ikiongozwa na Jaji mstaafu Aaron Ringera.

Jaji Muya alipinga uamuzi huo wa jopo la Jaji Ringera katika mahakama kuu na kurudishwa kazini na kuteuliwa Jaji.

Jaji huyo alidaiwa alivuruga uamuzi wa kesi ya Benki ya NIC iliyokuwa imeshtakiwa na walalamishi wawili katika mahakama kuu ya Bomey , Bw Alfred Kipkorir Mutai na Kipsigis Stores.

JSC ilielezwa na walalamishi hao kuwa jaji huyo aliahirisha kutoa uamuzi wa kesi yao kwa miezi mitano licha ya kufahamishwa magari waliokuwa wametoa kama dhamana kupokea mikopo yalikuwa yanauzwa kwa mnada..

JSC ilielezwa walalamishi walipata hasara kubwa kutokana na uzembe wa jaji huyo.

Tume ilielezwa Jaji Muya hafai kuhudumu katika idara ya mahakama kwa sababu ya utovu wa nidhamu.