Habari za Kitaifa

Jaji Grace Nzioka aitisha maji mawakili kupoza joto akisoma uamuzi

February 9th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

WAKATI Jaji Grace Nzioka aliketi kuanza kusoma ufafanuzi wa uamuzi wa mahakama kuhusu kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani, mwenyewe alikiri ilibidi azamie ushahidi kwa umakini wa hali ya juu.

Alisoma uamuzi huo dhidi ya mshukiwa mkuu Joseph Irungu almaarufu ‘Jowie’ na mwanahabari Jacque Maribe kwa ufasaha wa hali ya juu, huku akiwa amejibebea maji yake.

Isitoshe, alifahamu kwamba kikao cha uamuzi huo, uliochukua muda wa saa tatu na nusu, kilikuwa kipindi kirefu ambacho kingewakausha mawakili koo.

Hivyo, aliitisha maji na akaagiza mawakili wa upande wa mashtaka na wale wa upande wa washtakiwa wanakata kiu.

Jaji Nzioka yeye mwenyewe alionekana akimeza mafunda ya maji huku akitoa uamuzi wake ambapo Jowie alipatikana na hatia ya kumuua Monicah, huku Bi Maribe akifutiwa kosa hilo.

Kama dalili ya kuashiria matumaini aliyokuwa nayo kwenye uamuzi wa kesi ya shtaka la mauaji lililomkabili, Bi Maribe alivaa mavazi ya manjano.

Ni mavazi ya kupendeza, yaliyomvutia kila mmoja aliyemtazama. Hata wakati waliketi kizimbani na mshtakiwa mwenzake, Jowie, mwanahabari huyo alionekana mtulivu.

Baada ya wawili hao kuingia kizimbani, walizungumza kwa muda, na baadaye kila mmoja akaketi upande wake.

Wakati Bi Nzioka alianza kusoma uamuzi wake, korti nzima ilikuwa tulivu.

Washtakiwa wote walikuwa kimya, huku wakati mwingine wakiangaliana. Wote walionekana kuwa watulivu.

Hata hivyo, hali katika mahakama ilibadilika ghafla, wakati Jaji aliposema kuwa baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa kwao, ilikuwa wazi Jowie ndiye alihusika kwenye mauaji ya Bi Monicah Kimani.

Jowie alionekana kutoamini kauli ya Jaji Nzioka.

Aliangalia chini na kububujikwa na machozi. Alikuwa amefunika sehemu ya uso wake kwa barakoa nyeusi.

Jaji alisoma uamuzi wake kwa utulivu.

“Baada ya kutathmini ushahidi uliowasilishwa mbele yetu, mahakama haikumpata mshukiwa wa pili na hatia ya mauaji. Uamuzi na maoni ya mahakama ni kuwa mshtakiwa wa pili (Maribe) alishtakiwa makosa ambayo hakustahili,” akasema Jaji Nzioka.

Kuali hiyo iliyeyusha uso wa Bi Maribe na jamaa zake.

Wakati walipokuwa wakitoka kwenye mahakama, yaliyoshuhudiwa ni taswira za mchanganyiko wa hisia.

Bi Maribe alikumbatiana kwa hisia kali na babake, Bw Mwangi Maribe.

Walikumbatiana kwa muda wa kama dakika moja hivi.

Rafikiye mwanahabari huyo, bloga Dennis Itumbi, pia alikumbatiana naye kwa karibu dakika moja.

“Imekuwa safari ndefu iliyotupitishia hali ngumu kama familia. Tumeteseka kimawazo na kifedha. Hata hivyo, Mungu ametupigania,” alisema Bw Maribe.

Bw Itumbi alisema kuwa hatimaye haki imepatikana baada ya mwanahabari huyo “kuwekelewa makosa ambayo hakufanya”.

Hata hivyo, hali ilikuwa ya majonzi kwa familia ya Jowie.

Wakati jamaa na marafiki wa Bi Maribe walikuwa wakisherehekea, dadake Jowie aliangua kilio baada ya polisi kumweka pingu na kumpeleka korokoroni, akingoja kuhukumiwa mnamo Machi 8.