Habari za Kitaifa

Jaji Grace Nzioka atoa uamuzi dhidi ya Jowie kwa ustadi kama nyanya

February 9th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

JAJI Grace Nzioka aliyesikiliza kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani dhidi ya Joseph Irungu almaarufu Jowie, alionyesha weledi na ustadi wa hali ya juu alipoutoa uamuzi pasi kusoma daftari alilokuwa ameandaa la kurasa 170.

Mara aliwaitishia maji mawakili na hata yeye kwa vile alikauka ulimi kwa kuchambua uamuzi huo ilibidi anywe maji mara kwa mara.

Mara karani wake alikuwa anapaa katika meza yake kummiminia maji kutoka kwa flaski yake na mawakili waliletewa maji ya chupa na afisa wa kortini.

Jaji Nzioka alieleza kwa ufasaha uamuzi aliosema aliuandaa kutoka kwa kurasa zaidi ya 2,000.

“Nitasimulia uamuzi huu jinsi nilivyouandaa pasi kusoma neno baada ya jingine au aya baada ya nyingine,” Jaji Nzioka aliwaeleza washtakiwa, mawakili na watu wa familia za washtakiwa.

Jaji huyo alianza kueleza kwa mukhtasari ushahidi wa kutoka watu 35 waliofika kortini kutegua kitendawili cha mauaji hayo ya kinyama ya Monicah Nyawira Kimani ambaye alikuwa na umri wa miaka 28 alipokumbana na mauti ya kinyama.

“Nataka tuelewane sitasoma uamuzi wote neno kwa neno lakini nitasimulia barabara ushahidi ambao nimeuchambua,”alisema Jaji Nzioka.

Wote waliofika kortini walishangazwa na jaji huyo aliyeusoma uamuzi huo kwa ustadi na kusimulia sheria jinsi nyanya anavyosimulia hekaya kwa wajukuu wake.

Wakati wote ambao uamuzi ulisomwa Jowie na aliyekuwa mpenziwe, Jacque Maribe ambaye alikuwa mtangazaji katika kituo cha televisheni cha Citizen, walikuwa wanasoma habari katika skrini kwenye simu zao aina ya Smartphone.

Jacque aliinamisha uso wake huku Jowie akidondokwa na machozi huku akifuta machozi wa kiganja cha mkono baada ya kusikia mambo yanamwendea mrama.

Katika uamuzi huo, Jaji Nzioka alisema wote wawili Jowie na Bi Maribe walidanganya.

Alisema Bi Maribe alidanganya kwamba mpenziwe huyo (Jowie) alikuwa ameshambuliwa na majambazi usiku wa Septemba 20, 2018 lakini walinzi wa mtaa wa Royal Park Estate ulioko Lang’ata walitoa ushahidi tofauti.

Mtangazaji huyo aliandikisha taarifa kwa polisi kwamba Jowie alishambuliwa na majambazi lakini akabadili nia na kusema alijipiga risasi begani.

Kufuatia taarifa hiyo ya uongo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma huenda akamshtaki Bi Maribe kwa kudanganya polisi.

Jaji huyo alisema Jowie alidanganya pia alishambuliwa na majambazi.

Pia alidanganya kwamba jina lake ni Dominic Bisera Harun.

Jaji huyo alimwachilia Bi Maribe kwa shtaka la kuua na kumsukuma gerezani Jowie.

Baada ya kuachiliwa, kaka yake Monicah, Bw George Kimani alisema haki imetendeka.