Habari

Jaji Jessie Lesiit adinda kujiondoa kusikiliza kesi ya mauaji ya Sharon Otieno

July 19th, 2019 1 min read

Na MAUREEN KAKAH na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu inayosikiliza kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno imepuuza ombi la kuitaka ijitenge ikisema hakuna ushahidi uliotolewa kuonyesha kuna mwingiliano wa kimaslahi.

Sharon ambaye alikuwa mpenzi wa Gavana Okoth Obado wa Migori, aliuawa kinyama Septemba 3, 2018, akiwa na mimba ya miezi saba.

Msaidizi wa Gavana Obado, Michael Oyamo na karani wa kaunti Casper Obiero walikuwa wamewasilisha ombi lililosikilizwa Mei 29, 2019, ambapo walimtuhumu Jaji Jessie Lesiit kuwa na mwingiliano wa kimaslahi.

Akitoa uamuzi Ijumaa, Jaji Lesiit amesema hakuna sababu za kuridhisha kuthibitisha madai kwamba atashughulikia kesi hiyo kwa upendeleo wa aina yoyote inayolenga kuwaumiza washukiwa.

“Hakuna sababu za mgongano wa kimaslahi zilipeanwa zinazoweza kusababisha mahakama kujiepusha na usikilizaji wa kesi,” amesema Jaji Lesiit.

Katika ombi lao walalamishi hawa wawili walisema Jaji alikuwa ameonyesha mwegemeo upande mmoja kwa kumuachilia Obado kwa dhamana huku nao wakiendelea kuzuiliwa wakati huo “kwa sababu za kiusalama.”