Jaji Mkuu Martha Koome ateua majaji 3 kusikiliza kesi ya Sonko

Jaji Mkuu Martha Koome ateua majaji 3 kusikiliza kesi ya Sonko

NA RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu Martha Koome amewateua majaji watatu kusikiza na kuamua kesi iwapo Mike Sonko atakubaliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwania ugavana Mombasa.

Katika barua ambayo imemfikia wakili Dkt John Khaminwa, Jaji Koome ameeleza kuwa ameteua majaji watatu kusikiliza kesi ya Sonko.

“Afisi ya Jaji Koome imepokea faili ya kesi Nambari E27 ya 2022 kutoka Mahakama kuu Mombasa,” wakili katika afisi ya CJ Bw Muciimi Mbaka alisema katika barua aliyomwandikia Dkt Khaminwa Juni 29, 2022.

Bw Mbaka alifafanua kwamba Jaji Koome amewateua majaji watatu kusikiliza na kuamua kesi iwapo Sonko atawania Ugavana au la.

Kwenye barua hiyo majina ya majaji watakaosikiliza rufaa ya Sonko hawakutajwa lakini watasikiliza kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Mombasa

Jaji Olga Sewe aliyesikiza rufaa ya Sonko akipinga uamuzi wa kumzuia Sonko kuwania Ugavana Mombasa alisema “kesi hiyo imezua masuala mazito ya kikatiba yanayopasa kuamuliwa na majaji watatu.”

Jaji Sewe alikataa kumwagiza afisa wa uchaguzi kaunti ya Mombasa (CRO) Bi Swalha Ibrahim Yusufu amwidhinishe Sonko kuwania ugavana.

Bi Yusufu alikataa kumwidhinisha Sonko kuwania Ugavana akisema cheti cha Digirii cha Sonko kilikuwa na dosari kwa vile hakikuwa kimethibitishwa na chuo kikuu cha Kenya Methodist University (Kemu) alipowasilisha ombi la kuidhinishwa.

Pia Bi Yusufu alisema Sonko alitimuliwa Ugavana na Bunge la Seneti mnamo Desemba 20,2020 kwa ufisadi na ukiukaji wa maadili.

Kutokana na dosari hizo, Sonko alinyimwa fursa ya kushiriki katika kinyang’anyiro cha Ugavana Mombasa.

Sonko alikuwa ameteuliwa na Chama cha Wiper kuwa mwaniaji wake, Ugavana Mombasa.

Baada ya Sonko kunyimwa Ugavana Mombasa aliwasilisha rufaa mbele ya kamati ya IEBC ya kutatua masuala ya uteuzi (DRC).

DRC ikiongozwa na Wambua Kilonzo , Julius Nyang’aya na Irene Masitsi ilitupilia mbali rufaa ya Sonko akitaka uamuzi wa Bi Yusufu ubatilishwe.

Bw Wambua , Bw Nyang’aya na Bi Masitsi walikubaliana na uamuzi wa CRO kwamba Sonko hakutimiza masharti yaliyowekwa na IEBC na “kwamba hajahitimu kuwania Ugavana Mombasa.”

Chama cha Wiper kilichokuwa kimepinga uamuzi huo kilipewa muda wa masaa 72 kuanzia Juni 21, 2022 kumteua mwaniaji mwingine wa Ugavana.

Kufuatia agizo hilo kwa Wiper, Sonko alikishtaki akipinga kisimteue mwaniaji mwingine.

Katika rufaa aliyokata, Sonko alisema cheti cha Digrii kilichothibitishwa na Kemu kiliwasilishwa kama muda umepita.

Pia alisema amekata rufaa katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa kumtimua mamlakani alipokuwa Gavana wa Nairobi kwa madai alikuwa mfisadi na mtovu wa maadili.

Sonko anadai haki zake zimekandamizwa na IEBC na yapasa kushurutishwa kumwidhinisha kuwania Ugavana Mombasa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9,2022 uliosalia siku 39.

  • Tags

You can share this post!

Familia ya Cohen kutoa ushahidi zaidi

Wakuu wa Bhadala Jamat walaani vurugu zilizotokea katika...

T L