Habari Mseto

Jaji mstaafu aliyetorokea Uingereza asakwa kwa wizi wa mamilioni

July 18th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

JOPO linalosikiza kesi za utovu dhidi ya mawakili nchini jana lilimwondolea lawama wakili Virginia Wangui Shaw aliyekuwa amelaumiwa pamoja na Jaji mstaafu Philip Ransley anayeishi nchini Uingereza.

Na wakati huo huo hakimu mkuu Bw Francis Andayi ameamuru Jaji Ransley akamatwe na polisi wa kimataifa na kurudishwa nchini kujibu mashtaka ya wizi wa Sh 152milioni.

Mbali na kumwondolea lawama Bi Shaw, jopo hilo lililowajumuisha Bw Ezekiel Wanjama , Bi Grace Okumu na Bi Gladys Wamaitha liliamuru chama cha wanasheria nchini LSK limsake Jaji Ransley na kukabidhi samanzi za kufika mbele yake kujitetea.

Jaji Ransley alishtakiwa kwa wizi wa pesa hizo kutoka kwa mteja wake Bw Mr John Rowland Minns.

Jopo la wanachama watatu wa LSK lilimwondolea lawama Bi Shaw na kusema hakuhusika na kupotea kwa pesa za Bw Minns.

“Hii jopo limesoma makubaliano kati ya Bi Shaw na wakili wa Bw Minns yanayomlimbikizia lawama Jaji Ransley. Lawama dhidi ya Bi Shaw limefutiliwa mbali. Bw Minns ataendelea na kesi dhidi ya Jaji Ransley peke yake,” jopo hilo lilisema.

Bi Shaw alikuwa ameomba jopo hilp liondoe jina lake katika kesi hiyo akisema hakuhusika na mauzo ya shamba la Bw Minns.

Alisema Jaji Ransley aliuza shamba la Bw Minns kwa bei ya Sh277milioni na kumlipa baadhi ya pesa hizo na kusalia na Sh Sh152,702,850.17.

Jaji Ransley alikuwa amemweleza Bi Shaw kuwa alikuwa ametoa pesa katika akaunti ya kampuni yao ya Ransley McVicker & Shaw Advocates (RMS).

Katika ushahidi aliowasilisha mbele ya jopo hilo , wakili Shaw alifichua kulikuwa na makubaliano kati yake na Jaji Ransley kwamba mmoja wao anaweza kutoa pesa katika akaunti ya kampuni hiyo iliyoko katika benki ya Imperial. Jaji Ransley alimweleza Bi Shaw kwamba alitapeliwa pesa hizo na watu waliomdanganya kuwa watamuuzia Euro 13,700,000 kupitia kwa benki kuu ya Kenya (CBK).

“Jaji Ransley alimwagiza mhasibu wa kampuni yetu ya RMS kumtolea pesa katika akaunti ya benki ya Imperial na kumpelekea,” jopo limefahamishwa.

Wakili huyo alisema mnamo Agosti 2015 , Jaji Ransley alimweleza alikuwa ametoa pesa katika akaunti ya kampuni kwa matumizi yake.

Jopo hilo liliamuru kesi hiyo itajwe baada ya miezi minne LSK iifahamishe ikiwa imemkabidhi Jaji Ransley samanzi afike kujitetea.

Bw Minns anaomba jopo hilo limwagize Jaji Ransley amlipe pesa alizosalia nazo.