Habari Mseto

Jaji Sankale Ole Kantai ahojiwa na DCI

February 22nd, 2020 2 min read

Na PETER MBURU

JAJI wa Mahakama ya Rufaa Sankale Ole Kantai alihojiwa Ijumaa na maafisa kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI), kwa madai ya kuingilia kati kesi ya mauaji ya Tob Cohen.

Jaji huyo alikamatwa na kushinda katika makao makuu ya DCI kwenye barabara ya Kiambu, huku baadhi ya vyombo vya habari vikiripoti kuwa mkurugenzi wa DCI George Kinoti alivifahamisha kuwa Bw Sankale alikuwa akihojiwa kuhusu uhusiano wake na mshukiwa mkuu wa mauaji ya Bw Cohen, mjane wake Sarah Wairimu.

Wawili hao (Kantai na Wairimu) wanasemekana kuwa katika mazungumzo wakati wa uchunguzi wa mauaji ya Bw Cohen, huku ikiaminika kuwa jaji huyo alikuwa akijaribu kumsaidia kutokana na madai kuwa ndiye alimuua mumewe.

Vilevile, kukamatwa kwa Bw Kantai kulitokea siku ambapo gazeti la Daily Nation lilichapisha habari kuhusu jaji aliyedaiwa kuwa na mazungumzo ya kimapenzi na mpango wa kumuokoa mshukiwa wa mauaji kwa kumpa ushauri wa kisheria.

Katika gazeti hilo la jana, jaji mhusika (ambaye hakutajwa jina) alisemekana kuonekana katika baa ya Aqua Pool, katika hoteli ya Acacia Premier jijini Kisumu, ambapo alikuwa akimsubiri mshukiwa wa mauaji (ambaye pia hakutajwa).

Aidha, wawili hao walikuwa wakizungumza kwa simu, mara kwa mara kupitia jumbe fupi, mshukiwa akitafuta msaada wa jaji huyo, kabla ya polisi kuanza kumtafuta.

Walipopatana Kisumu, jaji huyo alikuwa akihudhuria kongamano -kulingana na nakala zilizoachwa katika chumba cha hoteli ambamo alikuwa, chumba nambari 405.

Mbali na mazungumzo yao yaliyodokeza uwezekano kuwa wawili hao walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi, ushahidi wa simu uliashiria kuwa jaji huyo ndiye aliyemlipia mshukiwa tiketi ya ndege kusafiri kutoka Nairobi hadi Kisumu kwa kutumia M-Pesa, na ni dereva wa jaji huyo aliyemchukua mshukiwa aliposhuka ndegeni.

“Habari ya asubuhi. Dereva ameondoka dakika tano zilizopita. Anakuja kukuchukua,” jaji akamwandikia mshukiwa.

“Sawa rafiki,” mshukiwa akajibu.

“Njoo na dawa ya kupulizia mbu ikiwa unayo,” jaji akaendelea kumwandikia.

“Nimefanya hivyo,” mshukiwa akajibu, na baada ya dakika chache akamtumia jaji ujumbe kuwa “dereva amenichukua”.

Alipofika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi mshukiwa pia alimtumia jaji ujumbe mfupi (SMS) kumfahamisha kuwa alikuwa akipanda ndege.

“Ulipata dawa ama nije na kitu nikishuka ndegeni…tunapanda sasa.”

“Nina dawa ya kukohoa na nyingine,” jaji akasema.

Katika mazungumzo haya, walikuwa wakitumia maneno na ishara nyingine za mapenzi, japo Taifa Leo haiwezi kuthibitisha ikiwa wawili hao walikuwa wakikutana kwa lengo la kimapenzi.

Katika hoteli hiyo, hakuna rekodi za kuonyesha kuwa mshukiwa alilala katika chumba tofauti, wala kuwa aliondoka siku hiyo. Pombe iliagizwa pia na kupelekwa chumbani hicho, kwa gharama ya jaji huyo.

Hadi keshoye saa kumi jioni wakati mshukiwa alipopigiwa simu na polisi akitakiwa kuripoti katika kituo cha Kilimani, wawili hao bado walikuwa pamoja.

Jaji alimlipia nauli ya ndege kusafiri kurudi Nairobi na akaondoka siku iliyofuatia.

Aidha, baada ya kuwasili Nairobi, mshukiwa anadaiwa kumtumia jaji ujumbe ambao polisi walirekodi akimtaka kuukagua na kufanya mabadiliko alipoona panafaa, kabla ya kuurejesha kituoni.

Kisa hicho sasa kimeamsha upya shaka kuwa kuna majaji waliopotoka kimaadili nchini na ambao wamekuwa wakishirikiana na washukiwa ama wahalifu kuvunja sheria na kukwepa haki.

Hata hivyo, hadi wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, DCI haikuwa imetoa habari rasmi kuhusu kukamatwa kwa Bw Kantai.

Bi Wairimu alikamatwa mnamo Agosti 28, 2019, siku chache baada ya maiti ya mumewe kupatikana nyumbani kwao.

Baada ya kukaa rumande siku 43, aliachiliwa kwa dhamana na tangu wakati huo amekuwa huru, japo anakumbana na kesi ya mauaji. Alishtakiwa rasmi mnamo Oktoba 3.