Habari Mseto

'Jaji' wa kipindi Vioja Mahakamani alivyouawa

December 13th, 2018 2 min read

Na HILLARY KIMUYU

MWIGIZAJI wa vipindi vya runinga Jamal Nassul Gadafi aliuawa kwa kudungwa kisu na mpenzi wake mnamo Jumanne usiku.

Marehemu Jamal, 39, anayefahamika kwa kuigiza nafasi ya ‘Jaji’ katika kipindi cha “Vioja Mahakamani” alidungwa kisu akiwa kwenye karamu katika hoteli ya Ark, eneo la Mlolongo.

Alipelekwa katika hospitali ya Shalom mjini Athi River ambapo madaktari walithibitisha kufa kwake.

Jamal alikuwa akishiriki kipindi cha Junior katika runinga ya KTN na juzi, alisajiliwa kushiriki kipindi cha Aunty Boss kinachopeperushwa kila Jumanne katika runinga ya NTV.

Kulingana na polisi, Jamal aligombana na mpenzi wake aliyetambuliwa kwa jina Grace Kanamu Namulo, 40 ambaye alichukua kisu na kumdunga. Chanzo cha ugomvi wao hakikujulikana mara moja.

Kisa hicho kiliripotiwa na msamaria mwema katika kituo cha polisi cha Mlolongo mnamo Jumanne usiku.

Mkuu wa polisi wa eneo la Athi River, Sharma Wario alithibitisha kisa hicho lakini akasema atatoa maelezo zaidi baadaye.

Bw Wario alisema polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya mwigizaji huyo.

Kwingineko, mwanamume mwenye umri wa makamo alijitia kitanzi karibu na boma la wakwe zake katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Daniel Chesang alikuwa amemfuata mkewe aliyetoroka na mali yake baada ya ugomvi wa nyumbani. Mwili wake ulipatikana ukining’inia kwenye mti katika kijiji cha Anin, Keiyo Kaskazini. Wakazi walisema Bw Chesang alifika katika kijiji hicho kutoka nyumbani kwao Kaunti ya Baringo akitaka kumchukua mkewe aliyerudi kwa wazazi wake wiki mbili zilizopita lakini akajitoa uhai kwa sababu ambazo hazikueleweka wazi mara moja.

Mkazi Eziline Kemboi alisema mke wa marehemu aliyetambuliwa kwa jina la Mercy Jepkemoi alienda kuishi na ndugu yake katika kijiji cha Anin baada ya kugombana na Chesang wakiwa katika Kaunti ya Baringo.

Alisema mkewe alikuwa amekataa kurudi kwake nyumbani kwao Kabartonjo.

Kamanda wa polisi wa utawala eneo hilo Joseph Biwott, alisema marehemu alijiua baada ya wazazi wa mkewe kukataa arudi nyumbani kwake.

Bw Biwott alisema huenda Chesang alijiua mnamo Jumatatu usiku akisema uchunguzi kubaini kiini cha tukio hilo tayari umeanza.

“Mwili wake ulipatikana na wanakijiji leo asubuhi na tumefahamishwa kwamba alitaka kurudi na mkewe kwao Baringo lakini wazazi wa mkewe walikataa,” alisema Bw Biwott.

Afisa huyo alisema mwili wa marehemu ulipelekwa mochari ya hospitali ya Iten ambapo utafanyiwa upasuaji.