Dondoo

Jamaa apiga demu teke kwa kudoea lishe huku akimkazia asali

May 21st, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KITHYOKO, MACHAKOS

KIOJA kilishuhudiwa  mtaani hapa kalameni mmoja alipomfurusha demu kutoka kwake akimlaumu kwa kuwa na tabia ya kudoea chakula chake na kumnyima asali.

Inasemekana jamaa alikuwa akimtongoza kidosho huyo kwa muda mrefu na kuambulia patupu.

Licha ya kukataa ombi la jamaa, demu alikuwa akimtembelea mara kwa mara na kupika alichotaka. Hata hivyo, jamaa alichoshwa na tabia ya demu huyo ya kumtembelea kila wakati kula mapochopocho na kumnyima asali.

“Kuanzia leo, sitaki  kukuona hapa kwangu. Nimekuwa mwema kwako kwa muda mrefu lakini hata hauna shukrani. Kila siku umekuwa ukinitembelea kula chakula changu lakini umeninyima raha kabisa.

Sitakuvumilia tena na nyumba yangu ione paa na uende ukaburudishe unaowapenda kama mimi siyo mtu wa maana kwako,” jamaa alilalamika.

Naye demu alijitetea lakini hakubadilisha msimamo wa polo.

“Usiwe na shaka, kila jambo huwa na mpango wake. Siku ikifika kila kitu kitakuwa shwari,” demu alisema. Jamaa hakuridhishwa na maneno ya demu huyo kisha akaamua kumburuta kutoka chumbani mwake.

“Hapana, sitaki vurumai zako. Toka nje mara moja. Wewe ni mtu bure kabisa. Unaniletea hasara na hakuna faida ninayoipata kutoka kwako,” jamaa alisema.

Jombi alidai kwamba demu alikuwa akifanya vipusa wamkatae wakidhani alikuwa ameoa.

“Unaniweka hasara mara tatu, kula chakula changu, kunikazia uroda na kunifanya nikataliwe na wenzako wanaodhani wewe ni mtu wangu,” aliwaka jamaa.
Ilibidi demu kuuma kona akihepa ghadhabu za jamaa huyo.

Hata hivyo haikujulikana iwapo jamaa alifanikiwa kupata kichuna mwingine wa kumridhisha.

…WAZO BONZO…