Dondoo

Jamaa ashtuka demu aliyedhani mlokole ni mlevi

February 1st, 2024 1 min read

NYALI, MOMBASA

Na JANET KAVUNGA

KALAMENI mmoja wa hapa alivunjika moyo baada ya kugundua kuwa, mrembo aliyetarajia kuoa alikuwa mlevi kupindukia.

Wawili hao walikutana katika hafla ya kanisa na jamaa akadhani alikuwa ameangukia chaguo la mke mwema katika maisha yake.

Waliendelea na uhusiano wao na kujivinjari huku demu akijifanya alikuwa mlokole hadi juzi jamaa alipomfumania akiwa amepiga mtindi hadi akawa hajitambui huku akiropokwa kuwa mpenzi wake ni sonko.

Jamaa alishangaa lakini marafiki wa demu wakamweleza hiyo ilikuwa tabia yake ya kawaida.

“Kwani haijawahi kumuona akiwa mlevi? Huyu ni bingwa wa kupiga sherehe na kubugia pombe. Anza kuzoea tabia yake,” demu mmoja alimweleza jamaa.

Haijulikani iwapo jamaa alimpiga teke au aliamua kuzoea tabia hiyo alivyoshauriwa.

***

Kisura motoni kudai maelfu ya ‘shopping’

AINAMOI, KERICHO

NA NICHOLAS CHERUIYOT

MWANADADA wa hapa alikosolewa kwa kiburi chake kilichowafanya watoto wake walale njaa hivi majuzi.

Kulingana na mdokezi, kipusa alipewa Sh3000 na mumewe akanunue bidhaa lakini akazikataa akiteta kuwa amezoea kufanya shopping ya Sh10,000 kila mwezi.

Jombi alichukua pesa hizo na kuenda kupiga sherehe pamoja na marafikize.

Kwa siku kadha mlo ukawa shida kupatikana bomani humo hadi jamaa wakaingilia kati. Demu alisutwa vikali kwa tabia yake.