Dondoo

Jamaa wazozania mahari ya dada

June 22nd, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

GATUNGA, THARAKA

KISANGA kilizuka katika boma moja eneo hili ndugu walipotwangana ngumi wakizozania mahari ya dada yao.

Jamaa walikuwa wakiishi mjini ila wakapanga safari waliposikia kuwa dada yao wa pekee alikuwa akilipiwa mahari. Kila mmoja wao alitaka kuonja kitu.

Baada ya mazungumzo ya muda, wakwe walikabidhi familia ya kidosho kitita kama mahari wakiahidi kurejea baada ya hafla ya harusi kuendeleza uhusiano kati ya familia zote mbili.

Jamaa aliyekuwa kifungua mimba ndiye alipokea hela kwa sababu baba yao aliaga dunia miaka kadhaa iliyopita.

Alidai kwamba baba yake mzazi alimwachia jukumu la kuwa kiongozi wa familia. Baada ya kumkabidhi mama yao sehemu ya pesa, jamaa alijitwalia zake na kuwapa ndugu zake Sh40,000 wagawane.

Hapo ndipo walizua kioja wakisema hawakuelewa jinsi alivyopiga hesabu na kumtaka kukoma kujipenda. Walidai kwamba wakwe waliwaachia Sh100,000 na jamaa alitwaa Sh50,000.

“Tumehangaika sana na dada kwenye shule tukilala njaa kwa kulemewa na karo. Inakuwaje unajipatia kiwango kikubwa cha pesa ukidai wewe ni kufungua mimba?” , jamaa waliteta.

Vuta nikuvute kati ya ndugu hao iliendelea kwa saa kadhaa na mwenzao alipokataa kubadilisha mawazo walianza kutumia mabavu ili kutetea walichodai ni haki yao.

Kwa hamaki, kifungua mimba alijaribu kujikinga na mzaha ukatumbukia usaha vita viliposhika kasi nusura watoane uhai kwa kurushiana ngumi.

Ilibidi majirani waingilie kati na kuzima vita vilivyokuwa vimechacha ila hakuna aliyejua hatima ya mzozo huo kwani jamaa alihepa na pesa hizo.