Jamaa za Obama wararuana mitandaoni

Jamaa za Obama wararuana mitandaoni

Na VALENTINE OBARA

NDUGU wawili wa aliyekuwa Rais wa Amerika, Barack Obama, Jumanne walianika tofauti zao za kifamilia peupe mitandaoni.

Bi Auma Obama na kakake, Bw Malik Obama walijibizana vikali kuhusu asili yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Malik, ambaye amekuwa hasimu wa Obama kwa miaka mingi, aliweka cheti feki kilichoonyesha kuwa rais huyo wa kwanza Mweusi wa Amerika alizaliwa Kenya.

“Umetekwa sana na wivu na machungu kwa kiasi kwamba unaweza kufanya chochote kile kumharibia kaka yako mdogo sifa! Kwa kuwa tu amekushinda kwa kila hatua ya maisha yake. Jitafutie sifa kwingine kakangu mkubwa,” akasema Auma.

Malik, anayeishi nchini humu hudai kuwa Obama hajali jamaa zake wanaoishi Kenya. Amekuwa akimshambulia kwa maneno licha ya kuwa walikuwa wandani wakubwa zamani walipokuwa vijana.

Hivi majuzi, alionyesha wazi kuegemea upande wa Rais Donald Trump katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika Amerika.

Mwanaharakati na wakili Miguna Miguna pia alimtaka Malik aachane na tabia ya kumwingilia Obama kila mara bila sababu.

You can share this post!

Ishara zote zaonyesha Waiguru ataepuka balaa

Wachina waliokuwa Kenya waruhusiwa kurudi kwao

adminleo