Makala

JAMAL GADAFI: Mpenzi alimuua kwa kumkataza kuwanengulia wanaume kiuno

December 13th, 2018 2 min read

COLLINS OMULO na PETER MBURU

ALIYEKUWA mwigizaji katika kipindi cha Vioja Mahakamani Jamal Nassul Gadafi alikumbana na mauti yake baada ya mzozo na mpenzi wake (pichani), kisha akadungwa kisu upande wa kushoto wa kifua mara moja hadi kufa, polisi wamesema.

Mgogoro baina ya wawili hao unasemekana kuanza wakati Bw Gadafi alitaka kujua ni kwa nini mpenzi wake huyo alikuwa akinengua kiuno na kukubali vinywaji alivyonunuliwa na wanaume ambao walihudhuria sherehe ya burudani katika hoteli ya Arks iliyoko eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos.

Wawili hao ambao wanasemekana kuwa katika uhusiano kwa miezi tisa pekee baadaye wanaripotiwa kwenda katika kichinjio kimoja karibu na hoteli hiyo ili kusuluhisha mgogoro baina yao, lakini badala ya suluhu kupatikana yakawa mauti.

Mwanamke huyo anasemekana kuchukua kisu na kumdunga mwigizaji huyo wa miaka 39, hatua iliyomsababishia kuvuja damu kwa wingi na kufa baadaye.

OCPD wa Athi River Sharma Wario alidhihirisha namna matukio hayo yalitendeka Jumatano.

Hata hivyo, afisa mmoja wa kituo cha Mlolongo alieleza Gazeti la Taifa Leo kuwa “kulingana na uchunguzi wetu, marehemu alihisi wivu alipoona wanaume wengine wakimnunulia mwanamke pombe. Hii ilipelekea vurugu ambazo ziliishia kwa mwanamke kumdunga kisu.”

Alisema kuwa walipokea habari kuhusu kisa hicho mwendo was aa nane usiku.

Bado polisi wanawasaka wanaume wawili ambao wanasemekana walimpeleka hospitali ya Shalom, kisha kuurejesha mwili eneo la tukio baada ya kusemekana kuwa alikuwa ameaga.

“Alidhibitishwa kufa wakati bado akiwa katika gari la washukiwa hao aina ya Toyota Axio,” afisa huyo akasema.

Alisema kuwa baada ya wanaume hao wawili kuuacha mwili katika gari, ni mwanamke huyo ambaye alimpigia bintiye simu kisha wakaupeleka katika hifadhi ya maiti, eneo la South C.

“Tulisambaza nambari ya usajili ya gari hilo ili litafutwe kisha tukalipata eneo la South C, japo lilikuwa limeisha mafuta kwa hivyo lilivutwa hadi kituoni na mshukiwa akakamatwa. Tuko naye seli,” akaendelea afisa huyo.

Alisema hata kisu kilichotumika kwa mauaji kilipatikana.

Mwanamke huyo atapelekwa hospitalini kupimwa akili, kabla ya faili yake kuwasilishwa kwa Kiongozi wa Mashtaka ya Umma ili afunguliwe mashtaka.

Hata hivyo, mwanamke huyo amekana kumuua Bw Gadafi, akidai kuwa aliangukia kisu kimakosa.

Rafikiye marehemu alikiri kuwa uhusiano baina ya wawili hao haujakuwa wa amani, kwani wamekuwa wakizozana.

Alisema kuwa marehemu alikuwa ametengana na familia yake tangu alipoanza uhusiano na mwanamke huyo takriban mwaka mmoja uliopita.

“Ni suala la mapenzi kwenda mrama. Mwanamke huyo alikuwa ameolewa, ana watoto wakubwa na hawakuwa wametalikiana na mumewe. Walikuwa na matatizo kuhusu hali ya maisha ya Jamal na namna alihusiana na wanawake wengine,” akasema rafikiye huyo, ambaye walikuwa wakiigiza pamoja.

Upasuaji wa maiti yake ulibaini kuwa kisu kilimdunga hadi kwenye moyo.

Mwili ulisafirishwa hadi Mombasa ambapo alitarajiwa kuzikwa Alhamisi.