Kimataifa

JAMAL KHASHOGGI: Mahakama yajiandaa kunyonga washukiwa watano

November 16th, 2018 2 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

WAENDESHA mashtaka katika kesi ya mauaji ya mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi katika makao ya ubalozi mwezi mmoja uliopita wanaitaka mahakama kuwahukumu kifo washukiwa watano kati ya 11 waliokamatwa.

Hii ni licha ya kuwa uchunguzi bado unaendelezwa dhidi ya watu wengine 10, japo wachunguzi wamemwondolea lawama mwanamfalme wa Saudi Mohammed bin Salim ambaye alikuwa akishukiwa kuamrisha mauaji ya mwanahabari huyo.

Uchunguzi huo umebaini kuwa mauaji hayo yaliamuriwa na afisa mmoja katika idara ya usalama Saudi ambaye alipewa kazi ya kumshawishi Khashoggi kurejea nchi hiyo.

Hii ilikuwa baada ya Bw Khashoggi kutoroka nchini humo na kwenda kuishi Marekani kwa kuhofia usalama wake, kutokana na kazi yake ya kumkosoa bin Salim kwa utawala wa kiimla.

Ripoti mpya sasa zinasema kuwa Bw Khashoggi alidungwa sindano yenye sumu baada ya kutofautiana na maafisa katika ofisi ya ubalozi nchini Instanbul, mnamo Oktoba 2.

Naibu mwendesha mashtaka Mkuu Saudi Shalaan bin Rajih Shalaan alieleza waandishi wa habari kuwa baada ya Bw Khashoggi kuuawa, mwili wake ulikatwa katwa na kupewa mshirika wa maafisa hao wa ubalozi ambaye ni wa Uturuki.

Hata hivyo, bado haijabainika mahali sehemu za mwili wa mwanahabari huyo zilipelekwa na asasi za usalama bado zinamsaka mshirika huyo.

“Uchunguzi wetu umebaini kuwa aliyeamuru mauaji ni kiongozi wa timu ya ushawishi aliyetumwa Istanbul na Naibu Mkurugenzi wa Usalama Generali Ahmed al-Assiri kumshawishi Khashoggi kurudi nyumbani,” Shalaan akasema.

Aliendelea kuwa bin Salman wakati wote huo hakuwa na habari kuhusu kilichokuwa kikiendelea.

Mwanawe bin Salman naye ametetea familia yake kutokana na mauaji hayo, akisema atakayepatikana na hatiya hafai huruma.

Hii ni licha ya kuwa amekosolewa kuwa uwezekano ni mkubwa alikuwa na habari kuhusu mpango wa mauaji hayo.

Hadi sasa, watu 21 waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo ni wale ambao wamekuwa maafisa katika asasi za usalama Saudi, ishara zikijitokeza kuwa ulikuwa mpango ndani wa kiserikali.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan naye amekuwa akisisitiza kuwa mauaji ya Khashoggi yaliamrishwa na wakuu wa serikali Saudia.

“Amri ya kumuua Khashoggi ilitoka kwenye mamlaka za juu kabisa za serikali ya Saudia,” akasema Erdogan, japo hakutaja wazi ikiwa ni bin Salman.

Serikali ya Uturuki bado haijaridhishwa na maelezo ya Kiongozi wa mashtaka, waziri wake wa masuala ya nje akisema mauaji ya mwanahabari huyo yalikuwa yamepangwa awali.

“Wanasema mtu huyu aliuawa kwa kuwa alipambana, lakini mauaji hayo yalipangwa kutoka awali,” akasema waziri huyo.

Tangu mwanzoni, serikali ya Uturuki imekuwa ikikosoa ile ya Saudi kuwa imehusisha hata waliomuua Khashoggi ndani ya timu ya wale wanaochunguza kuhusu kifo chake.