Kimataifa

JAMAL KHASHOGGI: Trump aionya Saudia kwa kuficha ukweli wa mauaji

October 24th, 2018 1 min read

MASHIRIKA Na CECIL ODONGO

RAIS wa Marekani Donald Trump ameyataja majibu ya serikali ya Saudia Arabia kuhusu mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi kama yasiyoridhisha na yanayoficha mengi machoni mwa jamii ya kimataifa.

Akizungumza na wanahabari katika Ikulu ya White House Jumatano Oktoba 23, Rais Trump alisema kwamba atahakikisha wanaohusika na kuficha habari kuhusu mauaji hayo wanakabiliwa vilivyo na Marekani.

“Mwanzo walitekeleza mauaji hayo kwa njia ambayo haingefichika na njia wanazotumia kukinga waliohusika ndizo duni zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya kuficha wauaji. Aliyetoa wazo hilo ajitayarishe kukabiliwa vikali nasi,” akasema Rais Trump.

Hata hivyo Waziri wa maswala ya nje wa Marekani Mike Pompeo baadaye aliunga mkono kauli ya kiongozi huyo akisema Marekani itawaadhibu wauaji wa mwanahabari huyo huku akitangaza kwamba serikali ipo katika mchakato wa kufutilia mbali visa vya washukiwa 21 ambao wametambuliwa na kudaiwa kuhusika.

Ufalme wa Saudia Arabia umukuwa ukitoa sababu zinazokinzana kuhusu mauaji ya Bw Khashoggi raia wa Marekani na mwanahabari wa jarida la Washington Post.

Baada ya wiki kadhaa ya kudai kwamba mwanahabari huyo alikuwa hai, serikali ya Saudi Arabia hatimaye ilikubali kwamba Bw Khashoggi, 59 aliuawa wakati wa oparesheni baada ya kufika katika ubalozi wa Uturuki kutafuta cheti cha kuvunja na ndoa yake ya awali ili kupisha ndoa yake na mpenziwe.