Kimataifa

Jambazi amvunja shingo ajuza wa miaka 100 kisha kumuibia

May 31st, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

DERBY, UINGEREZA

JAMBAZI alimshambulia mjane mkongwe mwenye umri wa miaka 100 na kumjeruhi vibaya alipokuwa akienda kanisani.

Ripoti zinasema Bi Sophia Kaczan alishambuliwa ghafla akavunjwa shingo na kupokonywa mkoba wake.

Ilisemekana alijikokota mwenyewe baada ya shambulio hilo na kuendelea kutembea hadi kanisani ambako alitafutiwa usaidizi.

Polisi walinukuliwa kusema majeraha aliyopata hayahatarishi maisha yake na wakatoa wito yeyote aliyeshuhudia kisa hicho ajitokeze kuwasaidia kusaka jambazi huyo.

Majirani wake walihuzunishwa na kisa hicho wakasema huenda aliyemshambulia alikuwa akitazama mienendo yake kwa muda mrefu. Hata hivyo, ilisemekana mkoba huo haukua na pesa.