Kimataifa

Jambazi ataka fidia ya Sh270 milioni kwa kupigwa risasi akiiba

May 31st, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

BROOKLYN, AMERIKA

JAMBAZI aliyepigwa risasi na mwenye duka alipopatikana peupe akipora duka la mvinyo, anataka alipwe ridhaa kwa majeraha aliyopata.

Inasemekana mwizi huyo alipatikana akiiba pombe katika duka lililo eneo la Long Island, Brooklyn alipopigwa risasi akijaribu kutoroka. Sasa amewasilisha ombi mahakamani kutaka alipwe ridhaa ya dola milioni 2.7 (Sh270 milioni).

Kwenye ombi lake, mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Shawn Harris alieleza kwa undani jinsi yeye na rafiki yake walivyovamia duka hilo mnamo Agosti mwaka wa 2016 kuiba pombe na mvinyo za bei ghali.

Mashirika ya habari yaliyochapisha ombi lake yalieleza jinsi alivyofichua kwamba mwenzake aliiba chupa nne za pombe naye akaiba chupa mbili ambazo alificha ndani ya suruwali.

“Tulienda kulipia chupa mbili na mwenye duka alipoulizia kitambulisho nilimwambia itabidi nikachukue ndani ya gari. Nilitoka nje na chupa nilizofucha zikaanguka. Tulifuatwa nje na mwenye duka akatoa bunduki na kuniambia nimrudishie chupa hizo,” akasema.

Ilisemekana walipigana na mwenye duka aliyekuwa akijaribu kuchukua funguo za gari lao ndipo akafyatua risasi. Alipata majeraha ya begani, na analalamika kwamba hakupokea matibabu bora kwa sababu alikamatwa punde baadaye.