Habari Mseto

JamboPay yaambiwa itulize boli

February 24th, 2019 1 min read

CECIL ODONGO Na COLLINS OMULO

KAMPUNI inayosimamia ukusanyaji wa mapato katika Kaunti ya Nairobi JamboPay italazimika kusubiri miezi tatu zaidi hata baada ya mkataba wake kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.

Kulingana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kaunti kuhusu bajeti Robert Mbatia, muda huo utaiwezesha serikali ya kaunti kutositisha oparesheni zake za ukusanyaji mapato.

Bw Mbatia alisema kwamba kamati ya muda itakayohusisha kikosi cha JamboPay, maafisa wa ukaguzi, teknolojia na wenzao kutoka Hazina ya Kitaifa watakutana kukubaliana jinsi kaunti na JamboPay watakavyoagana.

“Wakuu wa kaunti wanaonekana hawako tayari kuangazia namna itakavyoendeleza oparesheni zake baada ya kuondoka kwa JamboPay. Iwapo wataondoka ghafla leo tutakusanyaje fedha zetu?

Tunahitaji miezi mitatu na zaidi kujitayarisha kabla ya kuwaruhusu waondoke,” akasema Bw Mbatia ambaye ni diwani wa Kariobangi Kusini.

Kwa sasa serikali ya kaunti inatumia huduma za kielektroniki kukusanya mapato maarufu kama jijiPAY, huduma ambayo inamilikiwa na JamboPay iliyopewa mkataba na gavana mwaka wa 2014.

Diwani huyo hata hivyo alisema serikali ya kaunti ya Nairobi ililipa kampuni hiyo Sh30milioni ili kununua mashine na vifaa vya kuendesha oparesheni zake hata baada ya mkataba wake kukamilika.

“Kile ambacho naelewa ni kwamba tulilipa fedha kupokea huduma zao kwa muda wa miaka mitano. Hiyo inamaanisha kwamba lazima watatuachia mashine na mtindo wao wa oparesheni,” akasema Bw Mbatia.

Mnamo Januari 7 Afisa Mkuu wa kitengo cha Teknolojia ya kampuni hiyo Danson Muchemi alisema kwamba wapo tayari kuwaachia City hali machine, vifaa na mtindo wao wa oparesheni na akathibitisha kwamba watashirikiana na kampuni mpya kuhakikisha oparesheni za kaunti hazitatizwi.