Habari

James Nyoro atarajiwa kuapishwa Gavana mpya wa Kiambu

January 30th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SHEREHE za kumwapisha James Nyoro kuwa Gavana mpya wa Kiambu zitaanza Alhamisi mwendo wa saa nne za asubuhi, amesema mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi ya Naibu Gavana Damaris Wambui.

Haya yanajiri huku Gavana aliyeondolewa ofisini na Seneti, Ferdinand Waititu kusema atawasilisha leo Alhamisi mahakamani kutaka hatua hiyo ibatilishwe, akidai taratibu za kisheria hazikufuatwa.

Shughuli hiyo itaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu John Onyiego katika makao makuu ya serikali ya Kiambu, mjini Kiambu.

Miongoni mwa watakaoshuhudia sherehe hiyo ni Spika wa Bunge la Kiambu Stephen Ndichu na Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Wilson Wanyaga.

Bw Nyoro ambaye amekuwa Naibu Gavana anaapishwa saa chache baada ya seneti kuidhinisha hoja ya kumwondoa Bw Waititu ofisini iliyowasilishwa katika bunge hilo na bunge la kaunti ya Kiambu Desemba 23, 2019.

Hoja hiyo ilipitishwa mnamo Desemba 19, 2019 baada ya kuungwa mkono na madiwani 63 kati ya madiwani 92 wa kaunti hiyo.

Madiwani walidai Bw Waititu alishiriki ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka yake, ukiukaji wa Katiba na sheria nyinginezo, mashtaka ambayo yaliidhinishwa na Seneti.

Kati ya maseneta 38 walioshiriki upigaji kura Jumatano usiku 26 waliunga mkono mashtaka dhidi ya Waititu huku 12 wakipinga.

Akijitetea mbele ya Seneti, Waititu aliomba wabunge kutumia busara zao na wasimtimue kwa makosa ya jamaa zake.

Baada ya kuapishwa Bw Nyoro atahudumu kama Gavana kwa muda uliosalia na atakuwa huru kuteua naibu wake.

Madai ya ufisadi dhidi ya Waititu yamekuwa yakitolewa na madiwani wa kaunti ya Kiambu pamoja na wananchi kwa jumla huku baadhi wakiandaa maandamano ya kushinikiza kufutwa kwake.

Mwaka 2019 Waititu, mke wake Susan Wangari Ndung’u na binti yao, Monica Njeri walishtakiwa kortini kwa kuchukua zabuni ya Sh588 milioni bila ya kufuata sheria.

Mapema Jumatano Seneti ilikataa ombili la Waititu kuwasilisha ushahidi mpya wa kupinga hatua ya kuendelea kwa vikao vya kumtimua na hivyo kumpa nafasi ya kuendelea kuwa gavana.

Spika Kenneth Lusaka alipinga ombi hilo kwa kusema Bw Waititu hangeweza kuruhusiwa kufanya hivyo kwa kuwa muda wa kufanya hivyo ulikuwa umekwisha.