Habari Mseto

James Nyoro sasa kuapishwa rasmi kesho Ijumaa

January 30th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NI rasmi sasa kwamba James Nyoro ataapishwa rasmi Ijumaa awe Gavana mpya wa Kiambu baada ya kuondolewa afisini kwa Bw Ferdinand Waititu Babayao mnamo Jumatano.

Hii ni baada ya Katibu wa Kaunti ya Kiambu, Martin Mbugua kuchapishwa ilani kwenye toleo maalum la gazeti rasmi la serikali Alhamisi jioni akitangaza rasmi shughuli hiyo.

“Kwa mujibu wa kipengee 182 cha Katiba na sheria husika, natangazia umma kwamba sherehe ya kuapishwa rasmi kwa James Nyoro kuwa Gavana wa Kiambu itafanyika Ijumaa, Januari 31, 2020, katika Makao Makuu ya Serikali ya Kiambu kuanzia saa nne asubuhi,” akasema.

Awali, Jaji John Onyiego alisema kuwa hakuweza kuongoza sherehe hiyo kwa sababu ilani ya kufanyika kwa shughuli hiyo haikuwa imechapishwa katika gazeti rasmi la serikali na lile la Serikali ya Kaunti.