Habari

Jamhuri bila uhuru

December 12th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanapoadhimisha Sikukuu ya 57 ya Jamhuri Dei leo, mamilioni kati yao bado hawajaonja uhuru ambao mababu wao walipigania kwa kuteswa na kumwaga damu.

Kulingana na wananchi pamoja na wachanganuzi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa, uhuru ambao waliopigania ukombozi walitarajia umebaki ndoto, huku Kenya ikiendelea kushikiliwa kwa minyororo ya mataifa ya kigeni kwa usaidizi wa kundi ndogo la viongozi.

Kulingana na ripoti ya Taasisi ya Takwimu nchini (KNBS) ya mwaka huu, Wakenya 23.2 milioni wanaishi katika umaskini mkubwa. Hii inamaanisha kuwa watu hao hawapati chakula, elimu, usafi na makao bora.

Kulingana na ripoti hiyo, kuna ukosefu wa usawa katika kugawa rasilmali za umma, jambo linalofanya baadhi ya maeneo kuwa maskini zaidi kuliko mengine.

“Ni wazi kuwa miaka 57 baada ya wakoloni kuondoka, Kenya imepiga hatua chache kutatua matatizo yanayoivuta nyuma kimaendeleo,” asema Festus Kimonyi, ambaye ni mtaalamu wa uchumi.

Hali hii imezamisha matumaini ya Wakenya kuishi maisha ya heshima bila kuingiliwa ama kutegemea waliokuwa wakoloni ama wanasiasa.

Mtaalamu wa masuala ya kijamii Sheila Soila anasema ni jambo la kusikitisha kuwa miaka 57 baada ya uhuru, mamilioni ya Wakenya bado wanaishi kama maskwota katika nchi yao.

“Tunaona Wakenya wakifariki kwa njaa zaidi ya miongo mitano baada ya uhuru,” asema.

Kila mwaka Wakenya zaidi ya milioni tatu hukabiliwa na baa la njaa na utapia mlo, kulingana na shirika la Msalaba Mwekundu nchini.

Bi Soila anasema badala ya kustawi, sekta ya kilimo ambayo ingesaidia katika utoshelezaji wa chakula inaendelea kuzorota kutokana na sera mbovu, ufisadi na usimamizi mbaya.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, haki za maskini nchini zinaendelea kukiukwa, ambapo wanakosa huduma muhimu na kudhulumiwa asasi za haki wakiwemo polisi na mahakama.

Wachanganuzi wanaeleza kuwa chimbuko la Kenya kukosa uhuru kamili hadi sasa ni viongozi wake ambao wamepuuza sera za kuleta ustawi, na badala yake kuangazia maslahi ya kibinafsi, hali ambayo imejenga nchi ya kundi ndogo la mabilionea na mamilioni ya watu maskini hohehahe.

“Hii imefanya Kenya kuendelea kutegemea mikopo kutoka ng’ambo kufadhili miradi yake licha ya idadi ya walipa ushuru kuongezeka kila mwaka,” asema mchanganuzi Bw Kimonyi.

Kufikia Juni mwaka huu, Kenya ilikuwa ikidaiwa zaidi ya Sh7.2 trilioni na mataifa ya ng’ambo na deni hilo linaendelea kuongezeka.

Wataalamu wanasema itawachukua Wakenya zaidi ya miaka 40 kulipa madeni haya.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema itakuwa vigumu kuafikia uhuru wa kiuchumi ikiwa Kenya haitabadilisha sera za uongozi, kuangamiza ufisadi na kukumbatia utawala bora. Ingawa waanzilishi wa taifa la Kenya walitaka kuangamiza magonjwa, ujinga na umaskini, raia wa nchi hii wanaendelea kuuawa na maradhi yanayoweza kutibiwa kama vile malaria na kipindupindu, maelfu ya vijana wanakosa karo na mamilioni wanaishi katika umaskini mkubwa.

Mfumo wa afya nchini kwa sasa unakumbwa na matatizo makubwa huku kukiwa na uhaba wa dawa, misongamano hospitalini, uhaba wa madaktari na gharama ya juu ya matibabu, hali ambayo imechangiwa zaidi na ufisadi.

Wataalamu wa uchumi wanasema kwamba inasikitisha Kenya inategemea bidhaa na tekinolojia licha ya kuwa na watu walio na elimu na uwezo wa kubuni tekinolojia humu nchini.

“Mkoloni alienda lakini tulijifunga minyororo kwa kutegemea misaada, bidhaa na hata wataalamu kutoka nje kwa sababu ya kutoweka misingi halisi,” asema Bw Kimonyi.

Wachanganuzi wanasema kuwa viongozi wamekuwa wakiendeleza mbinu zilizotumiwa na wakoloni kujinufaisha kibinafsi kwa kusababisha migawanyiko ya kikabila.

Kijamii, Wakenya wangali wanaiga mitindo ya maisha ya kigeni tofauti na nchi nyingine zinazojivunia utamaduni wao.

“Tumetekwa na tabia za kigeni. Hatujivunii Ukenya wanavyofanya raia wa nchi kama India, Afrika Kusini, Nigeria na Rwanda,” asema Bi Soila.