Michezo

Jamie Vardy afungia Leicester katika dakika ya mwisho na kurefusha mkia wa Sheffield United kwenye jedwali la EPL

December 7th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Chris Wilder wa Sheffield United amesema mashabiki wa kikosi chake wana kila sababu ya kuvaliwa na hofu baada ya Leicester City kuwapiga 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Disemba 6, 2020.

Sheffield United walionekana kuwa ange kutia kapuni alama yao ya pili katika kampeni za EPL msimu huu baada ya Oli McBurnie kusawazisha mambo katika dakika ya 26 na kufuta juhudi za Ayoze Perez aliyekuwa amewapa Leicester uongozi kunako dakika ya 24.

Hata hivyo, Jamie Vardy, 33, alishirikiana vilivyo na James Maddison na kufungia Leicester bao la ushindi sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Vardy ambaye ni shabiki sugu wa Sheffield Wednesday ambao ni watani wakubwa wa Sheffield United, alimwacha hoi kipa Aaron Ramsdale na kusherehekea kwa mbwembwe na makeke yaliyomshuhudia akivunja kigingi cha kushikilia kibendera kwenye eneo la kupigwa kwa mipira ya kona.

Sheffield United almaarufu ‘The Blades’ sasa wana mwanzo mbaya zaidi kuliko kikosi chochote kingine katika historia ya kampeni za EPL. Timu hiyo imejizolea alama moja pekee kutokana na mechi 11 za hadi kufikia sasa na pengo la alama tano linatamalaki kati yao na West Bromwich Albion na Burnley.

“Hali inatisha. Iwapo wachezaji wanataka kusalia katika soka ya EPL, basi itawalazimu kufanya maamuzi bora,” akatanguliza Wilder katika kauli iliyopania kurejelea masihara yaliyofanywa na Chris Basham na John Fleck kabla ya Vardy kufunga bao la ushindi kwa upande wa Leicester.

“Tuna hofu kwa sababu matokeo yetu ni duni na mkia wetu unazidi kurefuka jedwalini,” akaongeza Wilder.

Wilder ambaye ameongoza Sheffield United kupandishwa ngazi hadi EPL mara mbili aliongeza: “Kwa sasa tunapoteza takriban kila mchuano nami ndiye kocha wa kikosi hicho kinachopoteza. Lazima hali ibadilike na tujitume zaidi dhidi ya washindani wengine.”

Ni matarajio ya kocha Brendan Rodgers wa Leicester kwamba matokeo yaliyosajiliwa na kikosi chake yatawapa motisha zaidi ya kuwapepeta AEK Athens katika mchuano wa Europa League utakaowakutanisha uwanjani King Power mnamo Disemba 10, 2020.

Sheffield United kwa sasa ndicho kikosi cha tisa katika soka ya Uingereza kuwahi kupoteza mechi 10 kutokana na 11 za kwanza kwenye msimu mmoja ligini. Katika EPL, kikosi hicho ndicho cha tatu baada ya Newcastle United mnamo 1977-78 na Manchester United 1930-31 kuwahi kupoteza idadi kubwa ya mechi (10) kutokana na 11 za ufunguzi wa msimu.

Baada ya kuwalika AEK Athens katika mchuano wao wa mwisho wa makundi katika Europa League, Leicester watakuwa wenyeji wa Brighton katika EPL mnamo Disemba 13 huku Sheffield United wakiwaendea Southampton ugani St Mary’s siku hiyo hiyo.