Jamii mbioni kulinda afya ya mama na mtoto

Jamii mbioni kulinda afya ya mama na mtoto

NA PAULINE ONGAJI 

Inakaribia adhuhuri siku hii ya Jumatatu, Agosti, 30, 2021. Joyce Nkalo, kutoka eneo la Embolei, Kaunti ya Kajiado, anawasili katika zahanati ya Oltepesi, iliyoko kaunti ndogo ya Kajiado Magharibi na mteja wake.

Bi Nkalo ambaye ni mkunga wa kitamaduni mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 47. Miaka miwili iliyopita, alibadilisha majukumu na kuwa msindikizaji wakati wa kujifungua, yaani ‘birth companion’.

Kinyume na awali ambapo kazi yake ilihusisha kuwazalisha wanawake wajawazito, kwa sasa kazi yake ni kuwaelekeza akina mama wajawazito hospitalini ili wajifungue salama.

Leo hii, Bi Nkalo amemleta Bi Lenkoi*, 25, kutoka sehemu za ndani za Oltepesi, ambaye anatarajiwa kujifungua wakati wowote.

“Huyu ni mtoto wangu wa nne lakini ni wa kwanza kujifungua hospitalini. Nilijifungua watoto wangu watatu kwa usaidizi wa mkunga wa kitamaduni,” aeleza.

Bi Nkalo amekuwa akifanya kazi hii kwa kipindi cha miaka miwili sasa, ambapo anaweza kuleta hata wanawake wajawazito watano hospitalini kila siku.

Awali, asema, hii haingewezekana hasa ikizingatiwa kwamba tokea jadi, wanawake kutoka jamii ya Wamaasai wamekuwa wakitumia huduma za wakunga wa kitamaduni wakati wa kujifungua.

Kulingana na Mami Kiperati, pia msindikizaji wakati wa kujifungua kutoka eneo la Oltepesi, mwanzoni haikuwa rahisi. “Lakini kutokana na sababu kuwa tuna uzoefu kama wakunga, wakazi wana imani nasi,” anasema

Suala la akina mama kujifungua hospitalini bado halijakubalika kikamilifu hapa, lakini wazo la kuwabadilisha wakunga wa kitamaduni kuwa wasindikizaji wakati wa kujifungua, limebadilisha mitazamo ya wengi, pasipo kusababisha mgongano wa kitamaduni.

“Licha ya kuwa tulitaka kuleta mabadiliko, hatukutaka kuzua ugomvi na jamii hii. Tuliamua kutumia watu wanaoaminiwa na jamii, hasa katika masuala ya uzazi. Hauwezi kuwalazimisha, kwani hautavishinda vita hivi,” asema Martha Nyagaya, Mkurugenzi wa shirika la Nutrition International hapa nchini.

Kwa kawaida, wasindikizaji hawa hupatikana katika kipindi chote cha ujauzito na wakati mwingi, mwanamke atasaka huduma zao kutokana na sababu kadhaa, kama vile hofu ya wahudumu wa kiafya, kukosa mbinu za usafiri kwenda katika kituo cha afya au kwa kushauriwa na jamaa.

Mbali na kuhakikisha kwamba akina mama wanazalia hospitalini, huduma za wasindikizaji hawa zinahusisha kutambua dalili hatari wakati wa ujauzito, vilevile kutoa taarifa muhimu kuhusu afya ya uzazi.

Huduma zao kadhalika zinaendelezwa hata baada ya mama kujifungua kwani huwafuatilia kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao kliniki.

Lakini mradi huu hauhusishi tu wasindikizaji wakati wa kujifungua. Kuna vitengo vya wanaume (Baba anzilisha) na wanawake (Mama anzilisha). Kitengo cha baba anzilisha kinahusisha kikundi cha wanaume ambao jukumu lao ni kuhakikisha kwamba akina mama wajawazito wanajifungua hospitalini.

Enock Simel na Isaac Ngongoni, 36 ambao ni wanachama wa mradi wa Baba Anzilisha, wamekuwa wakizuru sehemu mbalimbali wakieneza ujumbe wa kuhakikisha akina mama wajawazito wanaenda kliniki.

“Tunawahimiza kuwapeleka watoto wao kliniki na kukamilisha chanjo,” aeleza Bw Simel.

Mradi huu umekuwa na matokeo mazuri. Sheila Wambui, tabibu katika zahanati ya Oltepesi, asema kwamba idadi ya akina mama wajawazito wanaoenda kliniki imeongezeka hadi 70%.

“Hii ni kwa sababu ya shughuli za uhamasishaji, ambapo wanaelewa umuhimu wa huduma hizi za kiafya,” aongeza.

Kulingana na ripoti kutoka wizara ya Afya kuhusu kituo cha kiafya cha Oltepesi, idadi ya wanawake wajawazito walioenda kliniki, iliongezeka kutoka 166 mwaka wa 2017 hadi 440 mwaka wa 2020.

Aidha idadi ya wanawake waliokamilisha vikao vya kliniki wakati wa ujauzito, iliongezeka kutoka 17 mwaka wa 2017 hadi 277 mwaka jana (2020), huku idadi ya watoto waliozaliwa wakiwa hai ikiongezeka kutoka 6 mwaka wa 2017, hadi 261 mwaka 2020.

Lakini kando na kampeni kali za masuala ya ujauzito na kujifungua, wamekuwa wakiwafunza akina mama kuhusu masuala ya lishe wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua. Shughuli hizi pia zimekuwa na matokeo mazuri kwa upande wa lishe.

Kulingana na Godfrey Ogembo, Afisa wa lishe katika kaunti ndogo ya Kajiado Magharibi, kutokana na mazoea ya kutafuta huduma za kiafya kama vile kwenda kliniki wakati wa ujauzito, idadi ya wanawake wanaotumia vijalizo vya madini ya chuma na folic acid imeendelea kuongezeka.

“Idadi ya wanawake wajawazito waliopokea vijalizo vya madini ya iron/folate kwa ujumla, iliongezeka kwa takriban 100 % mwaka wa 2020,” aeleza.

Masuala ya lishe

Bi Nkalo asema mojawapo ya jukumu kuu la wasindikizaji wakati wa kujifungua ni kuhakikisha kwamba akina mama wanawanyonyesha watoto wao kwa miezi sita mfululizo, pasipo kuwapa chakula kingine.

“Suala la kuwanyonyesha watoto kwa miezi sita ni jambo geni miongoni mwa akina mama wengi wa Kimaasai. Kwa kawaida, pindi baada ya mama kujifungua, mtoto hupewa krimu maalum kutoka kwa maziwa ya mbuzi, kondoo au ng’ombe, ambapo bidhaa hii inanuiwa kudumisha afya ya mtoto wakati wote. Aidha, kuna aina nyingine ya krimu inayopewa mtoto mara mbili kwa siku ili kumzuia kuhisi njaa upesi, na hivyo kumwezesha mama kuendelea na kazi zake za siku pasipo usumbufu,” aeleza Bi Kiperati.

Pia kwa upande wa vikundi vya wanaume, suala la lishe bora limepewa kipaumbele.

“Kwa kawaida, chakula chetu cha kitamaduni huwa kinahusisha nyama na maziwa, ambapo kwa miaka mingi, wengi hawakutambua umuhimu wa kuhusisha mboga na matunda kwenye chakula chao cha kila siku. Tumewafunza kujumuisha vyakula hivi kwenye lishe yao,” asema Bw Simel.

Uchambuzi wa takwimu za utapiamlo uliotolewa mwezi Septemba 2021 na Halmashauri ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame, unaonyesha kwamba visa hivyo miongoni mwa watoto kati ya miezi 6 na 59 katika Kaunti ya Kajiado, vilikuwa 2930 ikilinganishwa na takwimu za kitaifa zilizofikia 142, 809, huku waliokumbwa na utapiamlo wastani vikiwa 11, 719.

Kwa upande mwingine, takwimu za visa vya utapiamlo miongoni mwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha katika Kaunti ya Kajiado vilikuwa 4, 896, kuwakilisha 5% ya jumla ya visa vya aina hii nchini kote.

Japo takwimu kutoka kituo cha afya cha Oltepesi zinaonyesha kwamba visa vya utapiamlo kwa ujumla vilipungua kati ya mwaka wa 2017 na 2020, miongoni mwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, viliongezeka kutoka 39 hadi 99 katika kipindi hicho.

“Hii ni kwa sababu wahudumu wa kiafya wa kujitolea wamepewa mafunzo ya kutambua utapiamlo na hivyo wamekuwa wakiewaelekeza wanawake wengi hospitalini,” aeleza Bw Ogembo.

Uchambuzi wa Halmashauri ya kitaifa ya kudhibiti ukame unaonyesha kwamba takwimu hizi katika kaunti zinazoonyesha viwango vya juu vya utapiamlo mkali, pia zinahusishwa na masuala mengine yasiyohusu chakula kama vile kutofikia huduma za afya na mbinu duni za kushughulikia watoto.

Kulingana na Bi Nyagaya, ingawa kuna vichocheo vingi vinavyosababisha utapiamlo miongoni mwa watoto, vile vile akina mama wajawazito na wanaonyonyesha, kwenda kliniki ni muhimu sana.

“Mbali na kuwa majukwaa ya akina mama kujifungua, hospitali na vituo vya kiafya vinatoa taarifa za lishe, na kutoa tiba ya matatizo ya kiafya yanayotokana na utapiamlo,” aongeza.

Ruth Nasinkoi, mratibu wa masuala ya lishe katika Kajiado asema kwamba hii ni mojawapo ya siri kuu ya kukabiliana na tatizo la utapiamlo pia katika sehemu zingine nchini.

You can share this post!

Mawakili wataka DPP atimuliwe

Shahbal apuuza ‘jeshi’ la Nassir

T L