Makala

Jamii ya Agikuyu Nairobi yapata kituo cha utamaduni mamboleo

May 10th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

TANGU jadi, masuala muhimu yanayohusu utamaduni wa jamii ya Agikuyu hufanyiwa katika eneo la Mukuruwe Wa Nyagathanga lililoko katika kijiji cha Gakuyu, Kaunti ya Murang’a.

Lakini katika siku za hivi punde, kumekuwepo malalamishi kwamba wazee wa jamii na wanasiasa wanalumbana, hali hii ikisababisha kuibuka kwa waliotaka ‘waanzilishi wa jamii’ (Gikuyu na Mumbi) kujengewa makao katika Kaunti ya Nairobi.

Katika kijiji cha Uthiru Ruthimitu, Kaunti ya Nairobi, kiongozi wa wazee katika jamii hiyo Bw John Mugwe Wanjuhi, aliambia Taifa Leo kwamba Mukuruwe Wa Nyagathanga katika Kaunti ya Murang’a ni eneo takatifu ambalo sasa limegeuzwa kuwa uwanja wa kuwanufaisha tu wanasiasa maarufu nchini.

Mzee John Mugwe Wanjuhi. PICHA | FRIDAH OKACHI

“Zamani eneo hilo takatifu lilikuwa na umuhimu mkubwa ambapo wanajamii walifika hapa kupata baraka, lakini biashara ambayo ilianza kufanyika pale, tuliona ni vyema kuwa na sehemu nyingine ya masuala ya kitamaduni hapa jijini Nairobi,” akasema Bw Wanjuhi.

Mzee huyo anaamini sasa jamii ya Agikuyu ina eneo jipya na la kisasa lakini linalowapa wanajamii fursa ya kujifunza na kudumisha utamaduni wao.

Wanaweza kuuonea fahari utamaduni wao wakiwa jijini Nairobi

“Kando na kufanya tohara kwa watoto zaidi ya 300, siku za Jumatano na Alhamisi sisi huruhusu watoto na wajukuu kuja hapa kujifunza vitanzandimi, vitendawili na methali za Gikuyu,” alisema Bw Mugwe.

“Nyumba hizi ambazo zinaashiria jinsi Gikuyu na Mumbi walivyoishi enzi zile ni za kisasa kabisa zikiashiria utamaduni. Aidha, wasichana huja hapa kufunzwa namna ya kupika chakula kinachoenziwa na jamii yetu,” akaongeza.

Katika kijiji hicho chenye ‘eneo takatifu jipya la jamii’, Bw Mugwe alianza kuonyesha eneo hilo ambalo lina milango mitatu kabla ya kufika sehemu maalum.

“Ukifika hapa, unaona mti aina ya Mugumo na hapa wanajamii hufanya maombi kwa Mungu wetu. Kisha unaingia lango la kwanza katika boma la Gikuyu na Mumbi. Ukiingia katika lango la kwanza unakuta kuna uwanja ambao ulitumika kufanya mazungumzo na wageni kutoka jamii nyingine,” akaeleza Bw Mugwe.

Kituo hicho ambacho kinaendelea kujengwa kitatumika kutoa mafunzo kwa vijana wa kizazi cha sasa ambao hawafahamu mengi kuhusu jamii yao.

“Ukifika lango la pili, hapa unakaribishwa kwenye boma la Agikuyu. Hii ina maana kuwa ukiingia basi una fursa ya kujieleza kilichokuleta hapa. Au ukiingia bila idhini ya kukaribishwa hii ina maana kuwa unataka kuanzisha vita,” akafafanua.