Afya na Jamii

Jamii yairai familia isiyoamini tiba za kisasa ibadili msimamo

February 16th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

FAMILIA moja katika eneo la Ngando, eneobunge la Dagoretti Kusini, haijakumbatia matibabu ya kisasa yanayopatikana hospitalini na kwa muda mrefu, wao hutegemea imani yao.

Familia hiyo iliyo na vijana watatu wanaofahamika kuwa wasanii katika mtaa huo, inaamini kizazi chao si cha kuchanganya matibabu wakati wa maumivu au mmoja wao anapougua ugonjwa wowote.

Bw Patrick Kamau, baba wa watoto wawili, alipewa idhini na familia kuzungumza ambapo aliambia Taifa Leo kwamba wazazi wao waliwaonya dhidi ya kuenda hospitalini na wangali wanaweka zingatio kwa walichoambiwa na wazazi wao.

“Nina umri wa miaka 36 na binafsi sijawahi kutembelea kituo cha hospitali au kuwa mgonjwa kutafuta matibabu. Mke wangu anapopata ujauzito, namkanda kuhakikisha mtoto aliye tumboni yuko salama. Ni mafunzo niliyopokezwa kutoka kwa familia,” akasimulia Bw Kamau.

Kulingana na Bw Kamau, familia yake imeshikilia kuwa tiba ya kisasa haiwezi ikafanya kazi iwapo hauna imani wanayotegemea.

“Acha nikuambie, hapa kijijini watu hutuita ‘marasta’ kwa kuwa na msimamo mkali wa kutotumia dawa za kisasa. Na hilo si kweli. Imani ya jamii yangu na kanisa langu hairuhusu kuchanganya mambo hayo mawili,” akaongeza.

Taifa Leo ilitaka kufahamu iwapo familia hiyo, hutumia Biblia wakati wa ibada yao ambayo hufanyika siku ya Ijumaa majira ya jioni.

“Tuna Biblia, hii ndio tunatumia sana wakati wa kuomba Muumba wetu,” akasema huku akionyesha nakala.

Majirani wake katika mtaa huo hushangazwa na jinsi familia hiyo inavyokosa kuhudhuria kliniki za wajawazito, wakitaja kuwa ni dhana potovu.

Wanakijiji wa Ngando wanaofahamu jamii hiyo. PICHA |FRIDAH OKACHI

Bi Christine Kavulani ambaye ni jirani wao kwa zaidi ya miaka saba sasa, alisema hajawahi kuwaona wakitembelea zahanati na wakati wa mazishi, jamii hiyo hukosa kushirikisha majirani kikamilifu.

“Kuna wakati mtoto wao aliumwa na mbwa na wakakataa kumpeleka hospitalini hadi serikali ikaingilia kati,” akasema Bi Kavulani.

Mzee wa Nyumba Kumi Meshack Nyabuto alisema hali ya maisha yao ilipeleka serikali kuingilia kati kuhakikishwa mtoto aliyeumwa na mbwa anapewa matibabu katika zahanati.

Mzee wa Nyumba Kumi Meshack Nyabuto. PICHA |FRIDAH OKACHI

Bw Nyabuto alisema haikuwa kazi rahisi.

“Tulilazimika kuchukua jukumu la kuhakikisha huyo mtoto anapelekwa hospitalini. Familia hiyo ilikaa ngumu lakini baada ya chifu kuwashika na kulala ndani siku mbili, walipata mtoto akiwa amepelekwa hospitalini,” akasema Bw Nyabuto.

Mhudumu wa kituo cha St Joseph Jecinta Njoki alisema kuwa watazidi kutoa hamasisho kwenye familio hiyo kuhakikisha kuwa wanaelewa umuhimu wa tiba inayopatikana hospitalini.

Kifungu cha 43 (1) (a) cha Katiba ya Kenya kinampa kila mtu kuwa na haki ya kupata kiwango cha juu cha afya kinachoweza kufikiwa, ambacho kinajumuisha haki ya kupata huduma za afya, ikiwa ni pamoja na huduma ya afya ya uzazi.

Kituo cha afya cha St Joseph ambacho hutoa hamasisho kwa familia hiyo kuhusu umuhimu wa tiba za kisasa. PICHA | FRIDAH OKACHI