Jamii yalia kitegauchumi kulemazwa

Jamii yalia kitegauchumi kulemazwa

Na KALUME KAZUNGU

UFUGAJI wa nyuki miongoni mwa jamii ya Waboni, Kaunti ya Lamu huenda ukaangamia endapo mikakati haitachukuliwa kunusuru.

Jamii hiyo tangu jadi imekuwa ikitegemea uvunaji asali, uchumaji wa matunda ya mwitu na uwindaji wanyama pori kujikimu maishani. Kwa miaka zaidi ya minane sasa, kumekuwa na changamoto tele, ikiwemo utovu wa usalama ndani ya msitu wa Boni.

Tangu operesheni ya kusaka magaidi msituni ilipozinduliwa na serikali kuu 2015, Waboni wamekuwa wakizuiliwa kuingia huko. Jaribio lao kuendeleza ufugaji wa nyuki katika maboma yao sasa limepata pigo, baada ya nyuki kutoroka kwa sababu ya kiangazi cha muda mrefu.

“Nyuki hutengeneza asali pahali ambapo pana maji na maua. Jamii ya Waboni inatambulika kwa kusambaza asali kwa wingi maeneo yote ya Lamu na nje ya kaunti hii. Inasikitisha kwamba kwa sasa haiwezekani,” akasema Bw Abatika Ali.

Bw Guyo Kokane alilalamika kuwa, baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yalikuwa yakiwafadhili Waboni kuendeleza ufugaji wa nyuki yalisitisha shughuli hizo tangu operesheni ya kusaka magaidi ilipozinduliwa na wanajeshi wa kulinda Kenya (KDF).

“Umaskini umekithiri eneo hili kutokana na kwamba kitega uchumi chetu ambacho ni ufugaji wa nyuki kimelemazwa. Isitoshe, ukame pia umekatiza matumaini yetu kwani wadudu hao wametoroka mizingani. Ningeomba serikali ituruhusu kuendeleza shughuli zetu za kijamii msituni,” akasema Bw Kokane.

Bi Khadija Musa alilalamika kuwa jamii hiyo imeguzwa kuwa ombaomba huku wakitegemea misaada kutoka kwa serikali na wahisani.

“Si uvunaji asali, uchumaji matunda au uwindaji wanyama pori. Vyote vimesambaratika tangu serikali itangaze marufuku ya kuingia msituni miakakadhaa iliyopita. Tumekuwa wa kutegemea misaada sasa. Misaada yenyewe haiji siku zote. Tunaumia,” akasema Bi Musa.

You can share this post!

Hofu ya tishio la kuua waumini

Asilimia 7 ya viwanda vimefufuka, idadi kubwa yasubiri 2023...

T L