Makala

Jamii yapinga kiwanda cha Sh12bn wakitetea mapango ya kitamaduni

February 12th, 2024 2 min read

VALENTINE OBARA NA MAUREEN ONGALA

BAADHI ya jamii zinazopakana na mapango ya Chasimba yaliyo kando ya barabara kuu ya Mavueni-Kaloleni, Kaunti ya Kilifi, wamepinga mipango ya ujenzi wa kiwanda cha utengenezaji simiti karibu na eneo hilo.

Kampuni ya Mashujaa Cement Plc iliweka bajeti ya Sh12.8 bilioni kwa shughuli nzima ya mradi huo, kuanzia kufanya utathmini wa kimazingira hadi ujenzi.

Ijapokuwa ripoti ya kampuni hiyo kuhusu Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Kijamii inaonyesha kuwa kiwanda kilichopangwa hakiko mahali halisi palipo na mapango hayo, wanaopinga mradi huo wanasisitiza kuwa, mapango hayo yataathiriwa na ulipuaji wa miamba.

“Mradi huu uko katika eneo la Pingilikani-Chonyi, eneo la Chasimba, Kaunti Ndogo ya Kilifi Kusini katika Kaunti ya Kilifi. Kampuni ya Mashujaa Cement Plc imepata fomu za idhini ya ardhi kutoka kwa jamii na kununua sehemu ya ardhi kutoka kwa wamiliki wa ardhi ya kibinafsi katika eneo la Chasimba,” kampuni hiyo ilisema katika ripoti yake.

Kulingana na kampuni hiyo, jamii zilizo karibu zitafaidika na fursa za kazi na shughuli nyingine za kiuchumi ambazo zinaweza kutokana na uwekezaji wake.

Ilieleza kuwa eneo lililochaguliwa halina rotuba nzuri kwa kilimo kwa sababu limejaa mawe.

“Hakuna maendeleo katika eneo linalopendekezwa la mradi. Eneo la mradi liko wazi na halina uzio na hakuna mipaka inayoonekana, na ardhi ina miamba,” kampuni hiyo inasema.

Katika barua iliyotumwa kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA), sehemu ya jamii inayopinga mpango huo inasema unahatarisha kuharibu urithi wao wa kitamaduni.

Waliotia saini wanadai kwamba hawakushauriwa kabla ya kutayarishwa kwa ripoti ya kutathmini mazingira na huo ulikuwa ukiukaji wa haki zao za kikatiba.

“Eneo ambalo Mashujaa Cement Plc inakusudia kujenga kiwanda chao cha simiti linazunguka eneo la kitamaduni liitwalo Mawe Meru ambalo ni muhimu sana kwa jamii na wahifadhi wa mazingira,” barua hiyo ya Januari 30, 2024 inasema.

Inaongeza kuwa, kuna uwezekano wa mizozo ya kifamilia kuibuka kuhusu uuzaji wa ardhi kwa kampuni, hofu ya uchafuzi wa mazingira na faida ndogo za kiuchumi kwa jamii za wenyeji.

Kulingana nao, viwanda kadhaa vimeanzishwa Kilifi lakini wenyeji hawafaidiki hasa katika suala la ajira.

Wanasayansi kadha kutoka Kilifi wamekuwa wakishinikiza mapango ya Chasimba yatambuliwe na kujumuishwa miongoni mwa Maeneo ya Urithi wa Duniani chini ya Umoja wa Mataifa.

Kulingana na watafiti, mapango hayo ni yanafaa kuhifadhiwa kwani kumewahi kupatikana mifupa ambayo inaashiria palitumiwa katika karne za kale.

Kwa msingi huu, wanasema hilo ni eneo ambalo linaweza kutumiwa vyema kwa manufaa ya kihistoria mbali na kuhifadhiwa kwa matumizi ya kitamaduni na vilevile, kuepusha uharibifu wa viumbe vya kipekee ambavyo vinapatikana hapo ikiwemo mimea na wanyama.