Habari Mseto

Jamii za maeneo ya mipakani zatakiwa zikumbatie Nyumba Kumi kukabili Covid-19

May 14th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya Alhamisi imethibitisha visa vipya 21 vya Covid-19, idadi jumla nchini Kenya ikifika 758.

Kati ya wagonjwa 21 hao, wanne ni madereva wa malori waliokaguliwa na kupimwa katika kituo cha mpakani Namanga.

Waziri msaidizi katika wizara Dkt Mercy Mwangangi pia ametangaza kwamba wagonjwa wawili wamefariki jijini Nairobi, idadi jumla ya walioangamia nchini kutokana na Covid-19 ikigonga 42.

Wagonjwa watatu wameripotiwa kupona, idadi ya waliopona nchini ikifika 284.

Maeneo ya mipaka yamekumbwa na changamoto katika vita dhidi ya usambaaji wa virusi vya corona na Dkt Mwangangi amesema serikali imeweka mikakati kuimarisha ukaguzi pamoja na ulinzi kuhakikisha hakuna anayevuka bila kupimwa.

“Tunaelewa mipaka imekuwa na changamoto nyingi. Serikali za mataifa ya Afrika Mashariki zinajadiliana kushirikiana kuona maambukizi ya mipakani yanadhibitiwa,” Dkt Mwangangi akasema akihutubia wanahabari Afya House, Nairobi.

Kituo cha mpaka wa Namanga kimekuwa kikimulikwa, kutokana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19 hasa miongoni mwa madereva wanaoingia nchini.

Visa vya raia wa taifa jirani la Tanzania kuingia nchini kupitia njia za mkato vimeripotiwa.

Ni kwa sababu hiyo ambapo Dkt Mwangangi amehimiza jamii zinazoishi maeneo ya mipakani kukumbatia mpango wa Nyumba Kumi kutambua wageni.

“Ninahimiza jamii zinazoishi mipakani zikumbatie Nyumba Kumi na kwamba akionekana mtu yeyote anayeshukiwa kuwa mgeni wakazi wa maeneo hayo watoe ripoti ili tusaidiane kudhibiti maambukizi zaidi,” akasema.