Habari Mseto

Jamii za Mlima Kenya zinakosa nguvu za kiume kwa kuabudu pombe na miraa – Nacada

June 4th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MAMLAKA ya Uhamasisho na Uthibiti kuhusu Ulevi na Utumizi wa Mihadarati (Nacada) imeonya kuwa pombe na miraa zitazidi kuponza jamii za Mlima Kenya uraibu huo usipokomeshwa. 

Ilisema kuwa kwa sasa wanaume wengi wa eneo hilo hawana uwezo wa kutunga wanawake mimba kwa kuwa nguvu zao za kiume zimemezwa na uraibu huo.

Afisa wa Nacada Mlima Kenya, Wilfred Gachuhi akiwa katika Mji wa Murang’a Jumatatu alisema kuwa kizazi cha eneo hilo hakina uhakika wa kuendelezwa kufuatia hali hiyo.

Alishikilia kuwa ikiwa serikali kuu na zile za Kaunti katika eneo hilo hazitazindua umoja wa kuangamiza ulevi, Miraa na ugoro katika jamii, basi kuna hatari kuu ya vijana wa eneo hilo.

“Tunaongea kuhusu janga kuu ambalo litajidhihirisha na jamii kukosa vizazi kufuatia wanaume wengi kukosa nguvu za kutungana mimba, kukosa maana ya ndoa na hatimaye mauti,” akasema.

Alisema kuwa kufikia mwaka wa 2017 eneo hilo la jamii za Gikuyu, Embu na Meru (GEMA) zilikuwa zimepoteza uwezo wa kuendeleza vizazi kwa zaidi ya watu 1.8 millioni kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

“Hawa ni wale ambao waliaga dunia kwa unywaji wa pombe kupindukia na pia watoto ambao hawakuzaliwa katika kipindi hicho kufuatia kulemewa na nguvu za kiume,” akasema.

Alisema hesabu ya watu na nyumba iliyofanywa 2010 ilionyesha upungufu huo kwani walitarajiwa kufikia zaidi ya Millioni nane lakini wakawa 6.3 milioni.

Hayo yalijiri huku waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i akizuru Kaunti za Kiambu na Murang’a hivi majuzi na kutangaza kuwa hakuna vile sheria za kuthibiti uuzaji na unywaji wa pombe zitalegezwa.

Alisema kulegezwa kwa sheria hizo ambazo zinatambuliwa kama Sheria za Mututho ni sawa na kuwaachilia wananchi kuendelea kujitia kitanzi katika vituo vya kuuziwa pombe.

“Vile tutafanya ni kukaza zaidi utekelezaji wa sheria za Mututho. Wewe kaa hapo ukisema korti lilisema lakini ujue nasi tuna usemi wetu na ambao hauendi kinyume na kazi ya mahakama. Wewe jitoe kafara uone nani ataumia,” akatisha.

Aidha, alimshukuru gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kupambana na ulevi kiholela katika Kaunti yake kiasi kwamba amepokonya baa zote leseni za kuhudumu na kuzindua mpango wa kuzipiga msasa upya.

Alisema kuwa atapunguza baa hizo kwa zaidi ya asilimia 60 wakati wa kutoa leseni mpya za kuhudumu.

Naye Dkt Matiang’i akamuunga mkono akisema kuwa serikali kuu iko nyuma ya Waititu katika mapambano hayo.

Waititu amekuwa akidai kuwa pombe haramu zilielekezwa katika jamii hizo miaka ya 80 kwa misingi ya siasa ambapo nia ilikuwa kuwamaliza kizazi.

“Ni lazima watu wa jamii hizi wajiulize mbona ni kwao tu pombe hizi zilikubaliwa ziuzwe bila ya kuthibitiwa. Na tangu maeneo yenu yafanywe kuwa kiwanda na pia soko ya pombe hizi, hamuzai na serikali inaashiria kuunganisha baadhi ya mashule kwani mengi hayana idadi ya kuhudumiwa na walimu 10,” akasema Waititu katika ziara hiyo ya Dkt Matiang’i.