JAMVI: Athari ya Uhuru kusema ‘fulani’ tosha

JAMVI: Athari ya Uhuru kusema ‘fulani’ tosha

Na BENSON MATHEKA

UAMUZI ambao Rais Uhuru Kenyatta atafanya kuhusu mrithi wake unaweza kusababisha mgawanyiko na misukosuko katika nchi hii au kuifanya kuwa thabiti zaidi.

Wadadisi wa siasa wanasema hii ni kutokana na karata ya kisiasa anayoonekana kucheza au washirika wake wanayoendesha kuamua atakayemrithi baada ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita, wengi walidhani kuwa angemuunga mkono naibu wake William Ruto hatua ambayo ingehakikisha kwamba chama cha Jubilee kinaendelea kutawala baada ya 2022.

Hii ilikuwa kauli yake wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka wa 2017 kwamba angetawala kwa miaka kumi na kumuunga Dkt Ruto kutawala kwa miaka kumi.

Hata hivyo, mambo yalibadilika aliporidhiana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na kumtenga Dkt Ruto katika masuala ya chama tawala.

Mgawanyiko katika chama hicho umefifisha matumaini ya Dkt Ruto kukitumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao huku Rais Kenyatta akimtaka ajiuzulu iwapo haridhiki na maamuzi ya serikali.

Wawili hao walitofautiana Dkt Ruto alipokataa kuchangamkia handisheki na kuikosoa vikali akidai ilinuiwa kumzuia kuingia ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao na mchakato wa kubadilisha Katiba wa BBI.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba ingawa Rais Kenyatta na Bw Odinga walifanya Wakenya kuamini kuwa BBI ilikuwa ya kuunganisha Wakenya, kuimarisha ushirikishi serikalini na kukomesha ghasia za baada ya uchaguzi, matukio ya hivi punde yanaonyesha huenda viongozi hao hawakuwa na nia moja.

“Kuna karata ambayo Rais Kenyatta anacheza na ambayo matokeo yake yanaweza kuacha Kenya ikiwa thabiti zaidi au kuvurugika zaidi. Kila hatua anayochukua na kauli anayotoa inakuwa kinyume na yanayotarajiwa,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Katana.

Anasema kwamba hatua yake ya kupokonya washirika wa Dkt Ruto nyadhifa za uongozi chamani na bungeni imezua mirengo miwili ambayo imekuwa ikilumbana huku wafuasi wa naibu rais wakilengwa, kukamatwa na kushtakiwa.

“Hatua hii inajenga hasira miongoni mwa wafuasi wa Dkt Ruto ambazo zinaweza kulipuka baada ya uchaguzi mkuu wa 2022,” asema Katana.

Wachanganuzi wanahisi kwamba Rais Kenyatta alimtumia Bw Odinga kumzima Dkt Ruto na kuafikia malengo yake kupitia BBI tofauti na ya kiongozi huyo wa chama cha ODM.

“Bw Odinga na wafuasi wake walidhani kuwa BBI ingemsaidia kuingia ikulu lakini baada ya mswada huo kupita awamu muhimu ya kupitishwa na bunge, tumeona mwelekeo mwingine huku kambi ya waziri huyo mkuu wa zamani ikihisi anachezewa shere. Hii inaweza kugawanya nchi hata zaidi,” asema mdadisi wa siasa Stevens Ouma.

Hali hii imesababishwa na hatua ya Rais Kenyatta kukumbatia viongozi wa vyama vingine vya kisiasa ambao wametangaza kugombea urais na ambao wandani wa Bw Odinga wanahisi hawakuwa sehemu ya handisheki.

Viongozi hao ni Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress, Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Gideon Moi wa Kanu, Charity Ngilu wa Narc na Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya.

Inasemekana kuwa Bw Odinga na chama chake cha ODM wanahisi kwamba Rais Kenyatta na maafisa wenye ushawishi serikalini wanapendelea muungano kati ya Mudavadi, Musyoka, Moi na Wetangula.

“Ikiwa madai ya ODM ni ya kweli, basi itabidi Rais Kenyatta abadilishe karata yake ndipo aepuke nembo ya msaliti wa kisiasa na kufanya nchi kugawanyika zaidi kinyume na kuchukuliwa kuwa alitumia BBI kutimiza malengo ya kibinafsi badala ya kuunganisha nchi,” asema Katana.

Aidha, kuwatenga wanasiasa hao katika BBI ili kumridhisha Bw Odinga, kutaashiria kwamba nia ya mchakato huo si kuunganisha nchi bali ni kuhusu siasa za 2022 tofauti na kauli za vinara hao.

Katana anasema kwamba itabidi Rais Kenyatta ajikune kichwa kuhakikisha kwamba msimamo wake kuhusu siasa za urithi haugawanyi Kenya zaidi.

“Hapa kuna rais ambaye amemsaliti naibu wake, anayekabiliwa na tetesi za kumchezea shere Bw Odinga na ambaye anaunga washirika wengine wanne wa kisiasa ambao wametofautiana na mshirika wake mkuu katika handisheki huku ikisemekana hana nia ya kubanduka katika siasa baada ya 2022. Ni hali ambayo kiongozi wa nchi anafaa kuishughulikia kwa uangalifu isitumbukize nchi katika msukosuko kama ule wa 2007,” asema Ouma.

Anasema kwamba mwelekeo ambao Rais Kenyatta atachukua kuhusu mrithi wake utaamua hali ya nchi baada ya 2022. “Kenya huwa ni nchi telezi sana,” asema.

Rais Kenyatta amelaumiwa na washirika wa Dkt Ruto na hata wa Bw Odinga kwa usaliti jambo ambalo wadadisi wa siasa wanasema linaonyesha wanahisi anataka kuamua atakaye mrithi.

You can share this post!

Rais apanga kuunda miungano ya amani

JAMVI: Raila anajitia hatarini kuhepwa ifikapo 2022