JAMVI: Bado sijaanza kampeni za 2022 – Ruto

JAMVI: Bado sijaanza kampeni za 2022 – Ruto

Na CHARLES WASONGA

WIKI hii, Naibu Rais William Ruto alionyesha undumakuwili kisiasa, wazi wazi pasi na kupepesa jicho.

Dkt Ruto aliwaacha Wakenya vinywa wazi alipodai kuwa hajaanza kampeni za kusaka kura za urais na kwamba ziara ambazo amekuwa akifanya kote nchini kuvumisha sera za chama cha United Democratic Alliace (UDA) ni za “kukagua miradi ya serikali kuu.

”Alishikilia kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haijatangaza rasmi kipindi cha kampeni na hivyo mikutano ambayo amekuwa akiandaa kila siku sio kampeni bali “majukwaa ya kukusanya maoni na hisia za Wakenya kuhusu miradi inayotekelezwa na serikali.

”“Ziara ambazo nimekuwa nikifanya kote nchini ni za kukagua miradi ya serikali bali sio kampeni. Na licha ya kwamba nimekuwa nikivalia mavazi yasiyo rasmi katika ziara hizo, hakuna sheria inayonilazimu kutelekeza majukumu yangu rasmi nikiwa nimevalia suti na tai,” akawambia wanahabari.

“Sijaanza kampeni kwa sababu IEBC haijatangaza rasmi kipindi cha kampeni. Kile ambacho ninyi huona nikifanya ni sehemu ya wajibu wangu kama Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya. Hii ni kuwatembelea wananchi, kusikiza maoni yao na changamoto zao na kukagua miradi ya maendeleo kama vile barabara,” Dkt Ruto akaeleza katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi, Jumatatu.

Alisema hayo baada ya kuongoza mkutano wa Baraza Shirikishi kuhusu Bajeti na Masuala ya Kiuchumi (IBEC), ambako mawaziri wanne walialikwa.Wao ni Ukur Yatani (Fedha), James Macharia (Uchukuzi), Peter Munya (Kilimo) na George Magoha (Elimu).

Ni waziri wa ugatuzi Charles Keter aliyefika katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na magavana tisa.Lakini kinaya ni kwamba baada ya Dkt Ruto kuongoza mkutano huo na kuhutubia wanahabari, alivua suti yake nyeusi na kuvalia fulani yenye rangi ya manjano kisha akafululiza hadi Narok kuendesha kampeni za UDA.

Hamna mradi yoyote ya serikali kuu ambayo alizindua wala kukagua katika ziara hiyo ambayo pia ilimfikisha katika eneo bunge la Belgut, kaunti ya Kericho. Ni katika eneo bunge hilo linalowakilishwa bungeni na Nelson Koech ambako alizindua madarasa katika Shule ya Upili ya Sikatuek.

Madarasa hayo yalijengwa kwa pesa za Hazina ya Ustawi wa Maeneo bunge (CDF).Duru ziliambia meza ya Jamvi la Siasa kwamba tangu mwaka wa 2019, imekuwa ni nadra kwa Dkt Ruto kufika katika Afisi yake iliyoko Jumba la Harambee Annex wala kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri.

Aidha, amekuwa akikwepa mikutano ya Baraza la Kitaifa kuhusu Usalama (NSC) na vikao vya mkutano wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Janga la Covid-19.Ni mwaka huu ambapo Dkt Ruto alidai kutengwa serikalini na majukumu yake kupewa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ambao alidai wamefeli katika majukumu hayo.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini Amri Kuu ambayo kwayo alibuni Kamati ya Mawaziri ya Kusimamia Ukaguzi na Utekelezaji wa Miradi ya Serikali Kuu. Kamati hii inayyoongozwa na Dkt Matiang’i ndio imekuwa ikiendesha kazi ya ukaguzi wa miradi kama hii katika ngazi ya kitaifa na kaunti.

Ni baada ya hapo ambapo Dkt Ruto aligeuza makazi yake ya Karen kama jukwaa la kukutana na jumbe za wanasiasa kutoka maeneo mbali mbali nchini kupanga mikakati yake ya kuwania urais 2022.Na juzi baada ya Rais Kenyatta kulegeza masharti ya kuzuia msambao wa ugonjwa wa Covid-19, Dkt Ruto amekuwa akiendeleza kampeni katika pembe zote za nchini akijinadi azma yake ya urais na sera za UDA.

Mikutano yake imekuwa ikihudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa UDA waliovalia mavazi manjano ambayo ni rangi rasmi ya chama hicho.Lakini wiki hii alidai kuwa majukwaa hayo huwa ni ya kushirikisha umma katika masuala ya serikali; hitaji muhimu la kikatiba .“

Mkiniona katika sehemu mbalimbali nchini, ni kwa sababu mimi ni Naibu Rais na miradi ya serikali imepatakaa kote nchini na hua nataka kupata majibu kutoka kwa wananchi kuhusu miradi hiyo,” Dkt Ruto akaongeza.Naibu Rais alisema ataanza kampeni rasmi baada ya IEBC kutangaza rasmi kipindi cha kampeni.

Kauli ya Dkt Ruto inajiri baada yake kukosolewa kwa kuzuru maeneo mbalimbali nchini akivumisha chama cha United Democratic Alliance (UDA) na ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.Vile vile, juzi Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliwashifu wagombeaji wa urais ambao wameanza kampeni za mapema akisema hiyo ni kinyume cha sheria.

You can share this post!

TAHARIRI: Taifa liige Kilifi kukabili mimba za mapema

Palmeiras wazamisha Flamengo na kutwaa taji la tatu la Copa...

T L